RAPA NAY WA MITEGO NA WEWE UNATAKA KIKI
NI True Boy tena, Emmanuel Elibariki maarufu kwa jina la Nay wa Mitego. Safari
hii amekuja na kibao chake kipya, Moto ambacho kama ilivyo kawaida
yake, ndani amewaponda wasanii wenzake, akiwataja kimafumbo, ambayo kwa
wanaofuatilia Muziki wa Kizazi Kipya wanaelewa anamzungumzia nani.
Lakini
achana na mafumbo kwa wasanii wenzake ambayo ni kama alama yake
kimuziki, kwa mara nyingine tena, ameweka maneno mengi yenye viashiria
vya matusi, hata kama siyo moja kwa moja, ila kwa watoto wa mjini,
wanaelewa.
Maneno kama Wapumbavu na
Kula kiboga, siyo maneno yenye tafsiri nzuri, hasa yanapotamkwa na mtu
anayesemwa kuwa ni kioo cha jamii. Nirejee tena, mimi ni shabiki wa Nay.
Napenda namna alivyojitengeneza kwa aina yake ya muziki. Lakini kama
mwandishi, ninatofautiana naye kwa namna anavyojaribu kuharibu taswira
yake kama msanii mkubwa.
Nay
ni mwanamuziki mzuri, anayejua vizuri kuitumia sauti yake na hata aina
ya midundo anayokwenda nayo, inamfaa kwa kiwango chake. Sijui, huenda
ndiyo kiki au hulka, lakini namuona ni kama msanii ambaye anatumia nguvu
kubwa kutoka nje ya mstari kuliko kukaa kwenye line! Utakumbuka ile
hatua ya kukamatwa kwake kwa ujio wa wimbo wake wa Wapo.
Kama si busara ya Rais Dk. John Magufuli,
leo hii tungezungumza kuhusu mambo mengine. Hii siyo sawa, ni mtu gani
anajiweka matatizoni kila mara kwa kuzungumza mambo binafsi ya watu
ambayo hayana tija kwa taifa? Kama hulka ya Nay ni mtu mkweli,
anayeguswa, mbona mashabiki wake wana kero nyingi tu? Kwa nini haimbi
kuhusu tabia ya wanasiasa kujipa uungu mtu wa kutaka mawazo yao ndiyo
yaheshimiwe kuliko wengine.
Wanapata
wapi ujasiri wa kujitamkia tu mtu aswekwe lupango kwa sababu tu
hawakupendezwa na maoni ya watu wengine? Mbona haimbi juu ya mashabiki
wake wanaouziwa vyakula feki katika maduka makubwa au hata uswahilini.
Vipi kuhusu nyimbo zenye kuwalenga wahubiri wapigaji wanaozidi
kumiminika kila siku hapa nchini? Kama ishu ni kuimba vitu vya ukweli,
hakuna haja ya kutaja majina ya wasanii wenzake ambao kimsingi hawana
madhara yoyote kwa jamii zaidi ya kujipa tabu wao wenyewe.
Watu
wanalalamika maisha magumu, bei za vyakula zinapanda, gharama za maisha
zinakuwa juu, lakini mishahara imebaki ileile. Kama ni ukweli, haya
ndiyo mambo ya kuimba ili wahusika wasikie na wafanyie kazi, kusudi
mashabiki wake wafaidike na hili litakuwa ni jambo jema, lakini
anachokifanya hakina tofauti na kile ambacho wenzake wanasema kiki
Kwani kwa mfano, kufifia kimuziki kwa mtu kama Young D, kuna
faida gani kwa shabiki ambaye anaishi Nyamongo, ambaye kila siku
anakimbizwa na askari wa migodini anapojitafutia mkate wake?
Nay,
wewe ni msanii mkubwa kutokana na uwezo wako wa kazi na kwa maana hiyo,
hizi kiki za kitoto ungeachana nazo, matusimatusi na maneno yasiyo na
maana yanapaswa sasa yasemwe na wasanii vijana wanaotafuta kiki ya
kutoka. Kila mtu huzaliwa, kutambaa, kutembea na hatimaye kukimbia na
katika hatua zote hizo zina tabia zake.
Ni
jambo la kuchekesha sasa kwa mtu kuishi na tabia za mtoto anayetambaa
wakati ni mtu mzima anayekimbia mwenyewe. Mtu anayejua anachofanya,
hawezi kutumia kiki ili kuhit, tunataka kazi mambo ya kitoto waachwe
watoto washughulike nayo.
No comments:
Post a Comment