KITAIFA:Tundu Lissu: Nitanyamaza Nikifa
Mwanasheria
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu,
ameachiwa kwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam
na kusema kuwa atanyamaza tu baada ya kufariki dunia.
Lissu
ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki na Rais wa Chama cha
Wanasheria Tanganyika (TLS), alipata dhamana jana baada ya mahakama hiyo
kubaini hoja za Serikali za kumnyima haki hiyo hazina mashiko.
Baada
ya kutoka mahakamani, alikwenda katika ofisi za Chadema zilizopo
Kinondoni, ambako pamoja na mambo mengine, alisema ataendelea kuikosoa
Serikali hadi pale atakapokufa.
“Hakuna
gereza litakalotunyamazisha, watu wakipelekwa mahabusu watazungumza
wakiwa mahabusu, wakifungwa watazungumza wakiwa kifungoni, hivyo ili
wanyamaze itabidi kwanza wafe… tutanyamaza tukiwa wafu kwa sababu wafu
hawasemi,” alisema.
Lissu alisema kuna haki ya kuwasema na kuwakosoa wale waliopewa madaraka na wananchi.
Alisema
katika sheria ya uchochezi ya mwaka 1953, kutoa kauli yoyote yenye
lengo la kukosoa matendo ya Serikali, sera si kosa na wala kumkosoa rais
na Serikali yake si kosa.
“Sasa
ukisema wanakukamata, wanakushtaki kwa uchochezi, wanakupiga,
wanakupeleka central (kituo kikuu cha polisi) au Oysterbay wakikupeleka
sio kosa, bali unatumia akili zako kuikosoa Serikali,” alisema Lissu.
Akizungumzia
kuhusu kupimwa mkojo, Lissu alisema alipelekwa na askari kwenye nyumba
iliyo karibu na Ocean Road, lakini alikataa kutekeleza hilo.
“Niliwaambia nyie maaskari mimi nimeshtakiwa kwa uchochezi, unathibitishaje uchochezi kwa kupima mkojo?” alisema Lissu.
Alisema askari hao walimjibu kuwa kuna vitu wanavitaka, akawaeleza: “Nendeni mkanishtaki, hamjapata oda ya hakimu, hamtaona mkojo wangu.”
Baada ya kauli hiyo, alisema askari hao walimwambia kuwa wao wana mamlaka.
“Nikawaambia
mimi ni Rais wa Mawakili (TLS). Siku ukikamatwa, ukaambiwa kupimwa
damu, mkojo waambie hutaki hata kama wamekushtaki.
“Ukitoa
mkojo na usiposaini hakuna dili, walichokuwa wanatafuta wapate dili ya
kutengeneza ‘headline’ (kichwa cha habari), ‘huyu anasema hivi kwa kuwa
anatumia dawa’, nani asiyejua polisi wanabambika? Nikakataa, nikawaambia
mnataka twende kunisachi twendeni.”
Lissu
alisema akiwa Segerea alikutana na wafanyabiashara James Rugemalira na
Harbinder Singh Sethi wanaokabiliwa na kesi ya uhuhumu uchumi na
utakatishaji fedha.
“Mwaka
jana nilisema hawa lile dili (kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow) watu
lazima wawajibike, waliowapa hela, waliosaini BoT (Benki Kuu ya
Tanzania), walioruhusu hizo fedha kwa kusema James Rugemalira na
Harbinder Singh wapewe wako wapi?” alihoji.
Lissu alihoji wapi walipo waliopewa mgawo wa fedha za Escrow.
Kabla
ya kutoa uamuzi wa dhamana jana, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, Wilbard Mashauri, alipitia hoja za pande mbili
zilizokuwa zinapingana, zilizowasilishwa mahakamani hapo mwanzoni mwa
wiki.
“Hii
kesi ina dhamana, hoja kwamba anakabiliwa na kesi nyingi zenye
viashiria va uchochezi haina mashiko kwa sababu hakuna taarifa kuwa
aliwahi kuruka dhamana.
“Kwangu
mimi hiyo haitoshi kumuweka mahabusu, hoja ya kwamba aendelee kuwepo
rumande kwa usalama wake, hakuna taarifa kwamba akipewa dhamana maisha
yake yatakuwa hatarini.
“Mshtakiwa
anawakilishwa na mawakili 18 wanaomuombea dhamana, wanafanya hivyo kwa
upendo walionao dhidi ya mshtakwa, hivyo haiwezekani akipewa dhamana
atadhurika.
“Mahakama
inakubali maombi ya dhamana, mshtakiwa atadhaminiwa kwa masharti ya
kuwa na wadhamini wawili, watasaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni
10 kila mmoja na mshtakiwa hatakiwi kusafiri bila kibali cha mahakama,”
alisema.
Baada
ya kutoa masharti ya dhamana, Hakimu Mashauri aliahirisha kesi kwa nusu
saa ili watafutwe wadhamini hao ambao walipatikana kwa juhudi za Wakili
Peter Kibatala aliyetoka nje ya mahakama kuwatafuta.
Awali
wadhamini hao walishindwa kuingia eneo la mahakama kutokana na
kuimarishwa kwa ulinzi kulikotokana na kuwapo kwa kesi za ugaidi
mahakamani hapo.
Kwa
upande wake, Wakili wa Serikali Mkuu, Simon Wankyo, alidai mahakamani
kwamba upelelezi wa kesi hiyo umekamilika hivyo aliomba tarehe nyingine
ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali.
Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 24, mwaka huu kwa kuanza usikilizwaji wa awali.
Lissu alidhaminiwa na wadhamini wawili walioweka dhamana ya maandishi ya Sh milioni 10 kila mmoja.
No comments:
Post a Comment