Wauaji wilayani Kibiti wadaiwa kutuma ujumbe kuwa wataendelea kuwauawa Polisi kwa sababu huwadhulum
Siku
mbili tangu kuuawa kwa polisi wawili wa Kikosi cha Usalama Barabarani
ambao walikuwa kazini katika Kijiji cha Bungu B, hali ya wasiwasi
imezidi baada ya wauaji hao kusambaza ujumbe unaoeleza kuwa wanaendelea
kusaka askari kwa kuwa ni wadhurumaji.
Watu
hao wametuma ujumbe mfupi uliondikwa kwenye karatasi na kisha kuutuma
katika mitandao ya kijamii, ukidai kuwa waliouawa (japo hawajatajwa
majina yao) walidhulumu watu kwa kutumia kazi zao.
“Tunawatangazia
wananchi tumewaua hawa kwa sababu wanadhulumu watu kwa kutumia kazi zao
na yeyote atakayefanya kazi hapa au nje ya hapa tutamtafuta hata
nyumbani kwake. Sisi tumejitolea kufa kuliko kuishi, kwa hiyo dereva au
raia popote uwaonapo toa taarifa iwe nyumbani au kazini,” unasema ujumbe huo.
“Hakuna njia ya kumaliza dhuluma isipokuwa chuma tu, hapa chuma tuuu!”
Ujumbe
huo ambao umeandikwa kwa mkono kwa kutumia kalamu ya rangi ya bluu
unadaiwa kuwa unazungumzia vifo vya askari polisi wawili wa Kituo cha
Polisi Kibiti, Sajent Salum na PC Masola waliouawa kwa kupigwa risasi
wakiwa kazini.
Mmoja
wa madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti (jina tunalo)
alisema ujumbe huo unawalenga askari wa kawaida na wa Kikosi cha Usalama
Barabarani.
Diwani huyo alisema kundi hilo linalofanya mauaji katika wilaya za Kibiti na Rufiji bado lipo na lina nguvu.
“Linaonyesha bado lina uwezo mkubwa wa kufanya mauaji na kutokomea kusikojulikana,” alisema.
Alisema
kwa sasa Serikali inapaswa kuongeza nguvu zaidi ya wapelelezi ili
kukomesha kikundi hicho ambacho hakijajulikana kinafanya hivyo kwa
sababu zipi na wala kinakojificha.
Akizungumzia ujumbe huo, kamanda wa polisi wa Pwani, Onesmo Lyanga alisema Jeshi la Polisi litaendelea kuwasaka.
“Tutapambana nao tu,” alisema Kamanda Lyanga na kukata simu.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment