Trending News>>

Sababu inayopelekea Hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa chafu

Mkurugenzi  wa Mafunzo  na Utafiti  Mwinyi Ussi Mselem amesema Hospitali kuu ya mnazi mmoja inakabiliwa na uhaba wa wafanyazi wa usafi hali ambayo  inachangia  kuzagaa kwa taka taka katika majengo hayo.
Akizungumza katika zoezi la Usafi  lililowashirikisha  wanafunzi  wa chuo  cha Biashara na Teknolojia  kilichopo  Mwanakwerekwe  amesema  kuwepo kwa baadhi ya  taasisi zinazojitolea kufanya usafi  katika maeneo mbalimbali ya kijamii ikiwemo Hospitali  kutasaidia kwa kiasi kikubwa   kuendelea  kutunza mazingira na kuziba nafasi za uhaba wa wafanyakazi.
Amesema  wanafunzi  wa chuo hicho  kuja kufanya  usafi  katika  eneo  hilo la hospitali  kuu kumeonesha  moyo  wa kizalendo na kuwapa hamasa viongozi  katika kuhakikisha  tatizo  la uhaba wa wafanyakazi  linapatiwa ufumbuzi  ili  hospitali hiyo iwe  katika  hali ya usafi  na salama  kwa wagonjwa.
Nae Mwakilishi wa Jimbo la Chukwani Mwanasha Khamis Juma amevitaka  vyuo na taasisi  za Serikali  na binafsi   kuwa na  moyo wa kizalendo  kujitolea   kufanya   shughuli za usafi  na kupanga  siku maalum  ya kufanya  usafi katika maeneo ya kijamii   Mijini na Vijiji kama vile, Hospitali, Masokoni, Katika Vituo vya kulelea watoto yatima, pamoja na maeneo  yaliyo wazunguka.
Mwanasha amesema  kufanya hivyo  itasaidia kuepusha maradhi ya miripuko katika vile kipindupindu na  mambo mengi   yanayochangia  maradhi kwa afya ya mwanadamu.
Kwaupande wake  mmoja  kati ya walimu wa chuo hicho Abdul-rahman  Saleh  Mohammed alifafanua lengo la  kufanya usafi katika maeneo  hayo ni  kuhakikisha   wanaunga  mkono jitihada za Serikali  pamoja na  wizara ya afya  ili Hospitali  ya mnazi moja iwe  katika  hali ya usafi  na mazingira bora.
Amesema usafi una  umuhimu wake  na  lazima jamii iwe na muamko wa kutunza na kudumisha mazingira katika maeneo yote yanayowazunguka na kuwacha kutupa taka ovyo na badala yake kutenga maeneo maalumu kwa  ajili ya kutupia taka zao ili kudhibiti   maradhi.

No comments:

Powered by Blogger.