Mwongozo wa vyeti vya kuzaliwa vilivyoandikwa kwa mkono waandaliwa..
Waziri
wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi ameuagiza Wakala wa
Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) kuandaa miongozo itakayowezesha
kuwaepusha Watanzania na usumbufu pindi wanapohitaji kutumia vyeti vya
kuzaliwa vilivyoandikwa kwa mkono.
Akizungumza
leo (Jumatatu) na wadau kuhusu usanifu mpango wa usajili wa matukio
muhimu kwa binadamu na ukusanyaji wa takwimu (CRVS), Profesa Kabudi
amesema amepokea malalamiko kutoka kwa watu kuhusu vyeti hivyo.
“Nimepokea
malalamiko kuwa kuna baadhi ya taasisi za Serikali na sekta binafsi
zinakataa kupokea vyeti vilivyoandikwa kwa mkono na badala yake
wanataka vilivyoandikwa kwa mashine,” amesema.
Profesa
Kabudi amesema mwongozo huo utasaidia watu kutokata tamaa kutokana na
usumbufu wanaoupata baada ya vyeti hivyo kukataliwa.
‘’Wanataka
vile vya kompyuta, mbona vyeti vya ndoa na vifo huwa vinaandikwa kwa
mkono, mtu wa kijijini anapata wapi kompyuta? Naomba mpokee na sitaki
tena kusikia malalamiko kuhusu kukataa vyeti vinavyoandikwa kwa mkono,’
’amesema.
Waziri
amesema Serikali imeamua kuboresha mfumo wa usajili uliopo na kuanzisha
utakaofanya kazi vizuri wa usajili wa matukio muhimu ya binadamu.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Rita, Profesa Hamis Dihengo amesema takwimu za sensa ya watu
na makazi za mwaka 2012 zinaonyesha kuwa asilimia 13.4 ya wananchi ndio
wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa.
Profesa Dihengo amesema idadi hiyo ni ndogo na ni kiashiria kuwa Serikali haina taarifa za idadi kubwa ya wananchi.
‘’Pamoja
na takwimu hizi wapo wananchi ambao huzaliwa na kufa bila hata taarifa
zao kuonekana katika kumbukumbu zozote za serikali, hivyo tunaomba
Watanzania wajitokeze kupatiwa vyeti vya kuzaliwa,’’ amesema.