Mauaji Kibiti: IGP Sirro Awataka Waandishi Kuwa Wazalendo
Wakati
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba akisema matukio ya
mauaji ya hivi karibuni mkoani Rufiji yana harufu ya kisiasa, Mkuu wa
Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro amevitaka vyombo vya habari
kuwa na uzalendo, ikiwa ni pamoja na kuacha kutoa taarifa zenye
kuchochea hofu kwa wananchi.
Waliyasema
hayo kwa nyakati tofauti juzi na jana katika mikoa ya Singida na
Morogoro. Waziri Mwigulu Akihutubia wananchi katika Kijiji cha Kaselya
wilayani Iramba, Singida juzi katika siku ya kwanza ya ziara ya siku
tatu kutembelea jimbo lake, Mwigulu alisema anahusisha mauaji hayo na
siasa kwa kuwa mauaji ya wananchi kwenye maeneo hayo yanawakumba zaidi
wafuasi na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alihoji; “Ujambazi gani huo wa Wana CCM tu? Hako kamchezo tumeshakagundua. Dhahiri, huo ni ushamba wa vyama vingi.” Alisema wanaodhani kuwa upinzani ni kwenye maisha wanakosea. “Naomba tupingane kwa kushindanisha sera na wala tusikunjiane ngumi kwa ajili ya siasa kwa kuwa siasa haipaswi kuwa ya uadui,” alisema.
Alisema
pamoja na siasa hazipaswi kuwa ya uadui bado wapo baadhi ya wapinzani
wanaotengeneza siasa ili zionekane kuwa ni za uadui. “Watu hawa
wangekuwepo wakati wa vita baina ya nchi yetu na Uganda, hakika
wangemsaidia Iddi Amin; bahati nzuri walikuwa bado wadogo,” alisema Waziri.
Sirro na uzalendo
Naye
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini, Sirro amevitaka vyombo vya habari
nchini kuwa na uzalendo ikiwa ni pamoja na kuacha kutoa taarifa zenye
kuchochea hofu kwa wananchi.
Alitoa
rai hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro
ambapo alisema baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikitumia maneno
yanayoongeza hofu kwa wananchi.
Kuhusu
mauaji yanayotokea katika wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga mkoani
Pwani, alisema vyombo vya dola vinaendelea kuyadhibiti na kwamba, jeshi
hilo linaendelea kuchukua hatua, lakini baadhi ya vyombo vya habari
vimekuwa vikitoa taarifa za kuchochea hofu.
“Taarifa zinazotolewa kwa umma hazioneshi kama kuna kazi inafanyika na vyombo vya dola kuzima mauaji hayo,” alisema
Aidha,
alisema pamoja na habari hizo kujenga hofu kwa jamii, pia zimekuwa
zikiambatana na picha za watu waliojeruhiwa, picha za silaha kuonesha
Pwani ni eneo la vita.
IGP
Sirro aliwataka wanahabari wanapoandika masuala ya kiusalama, watafute
ufafanuzi kwenye vyombo husika ili waandike taarifa sahihi, ikiwa ni
pamoja na kutanguliza uzalendo mbele huku wakitambua athari zinazotokana
na taarifa hizo kwa jamii.
Alisema wananchi wakijawa na hofu, watashindwa kutekeleza shughuli zao za kijamii na kiuchumi.
“Epukeni sana kuandika habari zenye sura ya kishabiki kwenye suala
hili, habari nyingi mnazoandika kwenye suala hili mnaonesha kama vile
mnalifurahia, hili si suala la kufurahia hata kidogo,” alisema
Alisema
hayo ni mapambano hivyo kila mmoja anawajibika katika kusaidia ikiwa ni
pamoja na kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kuzuia uhalifu na
kuwakamata wahalifu.
No comments:
Post a Comment