KOCHA MKUU WA STARS MAYANGA ATANGAZA KIKOSI CHA COSAFA
Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.
Kocha Mkuu wa timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Salum Shabani
Mayanga, leo Jumatano Juni 14, 2017 ametangaza majina ya wachezaji 22
watakaounda kikosi kinachokwenda kushindana kuwania Kombe la Castle
Cosafa nchini Afrika Kusini.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Bia ya Serengeti, inatarajiwa kuanza
kambi rasmi kesho Jumapili Juni 18, mwaka huu. Kambi hiyo itakuwa
kwenye Hoteli ya Urban Rose, iliyoko Mtaa wa Jamhuri katikati ya jiji la
Dar es Salaam.
Afisa habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF) Alfred Lucas
amesema kuwa kikosi hicho ambacho kimechaguliwa kimeweza kuongeza baadhi
ya wachezaji wengine ikiwa pia ni katika kukiandaa kikosi hicho kwa
ajili ya Michuano ya Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).
Lucas amesema Taifa Stars inajiandaa na michuano ya Cosafa
inayotarajiwa kuanza Juni 25, mwaka huu. Michuano hiyo, inaandaliwa na
Baraza la Mpira wa Miguu la nchi za Kusini mwa Afrika ambako Tanzania -
mwanachama wa Cecafa, imepata mwaliko kushiriki.
Tanzania imepangwa kundi A ambako wapinzani wake ni Mauritius,
Malawi na Angola wakati Kundi B ni Msumbiji, Shelisheli, Madagascar na
Zimbabwe. Timu za Botswana, Zambia na Afrika Kusini kadhalika Namibia,
Lesotho na Swaziland zitakuwa na mechi maalumu (play off) ili kuingia
robo fainali.
Lucas amesema kwa mujibu wa Mayanga, kikosi hicho kinaundwa na
makipa Aishi Salum Manula (Azam FC), Benno David Kakolanya (Young
Africans SC) na Said Mohammed Said (Mtibwa Sugar FC).
Walinzi wa pembeni upande wa kulia ni Shomari Salum Kapombe (Azam
FC) na Hassan Hamis Ramadhan ‘Kessy’ (Young Africans SC) wakati upande
wa kushoto wapo Gadiel Michael (Azam FC) na Amim Abdulkarim (Toto
Africans FC).
Walinzi wa kati ni Erasto Nyoni (Azam FC), Salim Hassan Abdallah
(Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba SC) na Nurdin Chona (Tanzania Prisons)
wakati viungo wa kuzuia kuwa ni Himid Mao (Azam FC) na Salmin Hoza wa
Mbao FC.
Kadhalika wako viungo wa kushambulia ambao ni Mzamiru Yassin
Selembe (Simba), Simon Happygod Msuva (Young Africans SC), Raphael Daudi
(Mbeya City) na Shizza Ramadhani Kichuya (Simba SC).
Katika safu ya ushambuliaji wamo Thomas Emmanuel Ulimwengu (AFC
Eskilstuna – Sweden), Mbaraka Abeid Yusufu (Kagera Sugar), Stamili
Mbonde, Elius Maguli (Dhofar SC) na Shabani Idd Chilunda (Azam FC).
No comments:
Post a Comment