Kichanga chateketea kwa moto
Mtoto Faraja Simon mwenye umri wa
mwezi mmoja amefariki dunia baada ya chumba alicholazwa kuteketea kwa
moto katika Kijiji cha Mbela, wilayani Misungwi mkoani Mwanza.
Akizungumza
na wanahabari leo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Ahmed Msangi
amesema tukio hilo limetokea juzi Juni 18, 2017 saa 1:00 jioni, ambapo
amedai kuwa marehemu alikuwa akiishi kwa mama mlezi aliyefahamika kwa
jina Bi. Eva Mnari (37) baada ya kufiwa na mama yake mzazi mwezi
uliopita.
Kamanda Msangi amesema siku ya tukio
hilo mama mlezi alimlisha mtoto huyo chakula na kisha kumpeleka chumbani
kulala na kutoka nje kuendelea na shughuli nyingine.
Amesema wakati mama huyo akiwa nje,
aliona moto na moshi mwingi ukitokea chumbani alimolala marehemu ndipo
aliita watu waje kumsaidia kuuzima moto huo lakini moto ulikuwa
umeunguza godoro alilokuwa amelazwa marehemu na kumuunguza hali
iliyopelekea marehemu kupoteza maisha papo hapo
Kamanda Msangi ameendelea kusema kuwa
mpaka sasa bado chanzo cha moto huo bado hakijafahamika na kwamba
upelelezi unaendelea kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali
kuhusiana na tukio hilo