BINTI ASIMULIA JINSI ALIVYOBAKWA KWA ZAMU NA DEREVA NDANI DALADALA MJINI MOSHI
Dereva na kondakta wa daladala zinazofanya safari ndani ya Manispaa ya
Moshi mkoani Kilimanjaro, Soweto–Mbuyuni wanatuhumiwa kumbaka abiria wao
kwa zamu na kumuumiza sehemu za siri.
Tukio hilo lililotokea Juni 12 saa moja jioni maeneo ya Veta katika
uchochoro uliopo karibu na shule ya Northen Highland iliyo umbali wa
mita 400 kutoka barabara ya lami.
Akielezea tukio hilo, binti huyo mwenye umri wa miaka 20 alisema
alitumwa na bosi wake kwenda kununua mahitaji ya nyumbani Soko la
Mbuyuni na kumuelekeza kuwa akimaliza apande basi la Soweto sokoni hapo
na ashukie mwisho ambako angechukua bodaboda ya kumfikisha nyumbani.
“Nilipomuuliza konda akaniambia ndiyo na nikampigia bodaboda ambaye
nilipewa namba na bosi wangu ili ampe maelekezo huyo kondakta sehemu
ambayo watanishusha ili yeye anichukue hapo na wakazungumza na baadaye
akanirejeshea simu yangu,” alisema msichana huyo.
Alisema baada ya hapo safari ya kutoka Mbuyuni kwenda Soweto ilianza.
“Kwa kuwa nilikuwa mgeni, sikuelewa hata kituo kipi cha kushukia.
Niliendelea kukaa hadi nilipoona watu wote wameisha kwenye (Toyota)
Hiace, ndipo nikamuuliza konda kwa nini hanishushi akasema bado
sijafika,” alisema.
Anasema alishangaa kuona dereva anaenda kuegesha gari uchochoroni na aliposimama, kondakta akashuka, akidai anaenda kujisaidia.
“Aliporudi kwenye gari alifunga mlango na wakazima taa na kuanza
kuniambia kuwa wamenipenda kama ninataka kuwa hai nikubaliane na
wanachokitaka na nikikataa wataniua,” alisema binti huyo.
Alisema baadaye dereva alitoka kwenye usukani na kumfuata alipokaa na kuanza kumpapasa.
Alisema alipoona hivyo alijaribu kutoka nje kupitia dirishani, lakini
walimvuta ndani huku wakimfunga mdomo asipige kelele na kumtishia
kumuua.
“Nilikubali yaishe na nikatulia. Akaanza dereva huku kondakta akinishika
mikono na baada ya kumaliza alichofanya, konda naye akaja akafanya
hivyo hivyo. Nilisikia maumivu, lakini nilishindwa kupiga kelele kwa
kuwa walinitisha kuwa wangeniua,” alisema dada huyo.
“Walipomaliza kufanya ukatili huo, konda alimwambia dereva kuwa waniue
kwa kuwa nimeshawatambua, lakini dereva akasema hakuna haja.”
Alisema katika mabishano hayo alijikaza na kuwaambia kuwa yeye ni mgeni
na hajui popote kwa hiyo hatamwambia mtu kwa kuwa hilo ni tukio la aibu.
“Walikubaliana na mimi na wakaniambia kuwa ni kweli kubakwa ni kitendo
cha aibu kwa hiyo nikimwambia mtu nitatengwa na jamii. Nikawaomba
wanisaidie sehemu ya kupata msaada niweze kufika nyumbani,” alisema.
Alisema baadaye aliwaomba aende kuchukua kiatu chake kilichokuwa
kimedondoka dirishani wakati akitaka kuruka, na walipomruhusu akatumia
nafasi hiyo kusoma namba za gari.
Mlezi wake, Abdi Massawe alisema baada ya kufika nyumbani akiwa na
bodaboda, binti huyo alimweleza tukio hilo na akatoa taarifa polisi
ambako alipewa fomu ya matibabu aliyoitumia Hospitali ya Mawenzi, ambako
vipimo vilithibitisha kuwa alibakwa.
“Huyu binti ni mgeni kutoka mkoani Singida. Hapa Moshi ana mwezi mmoja tu,” alisema Masssawe.
Massawe alisema baada ya hapo alianza kusaka daladala hilo kwa kutumia
namba alizopewa na binti huyo na kufanikiwa kuikuta maeneo ya Soweto.
Baadaye aliwapigia simu polisi ambao walifika na kushusha abiria
waliokuwamo na kuipeleka kituoni.
Alisema wakati dereva akiendelea na mahojiano kondakta alitoroka.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Koka Moita alisema derava
wa gari hilo aliyemtaja kuwa ni Salimu Abdalla (30) anashikiliwa na
polisi ambao wanaendelea kumtafuta kondakta ambaye alitoroka akiwa
katika kituo cha polisi.
Kwa sasa binti huyo anatibiwa Hospitali ya Mawenzi.