Trending News>>

Bifu la Ronaldo na Mourinho latajwa akitua Man United

NI vigumu kuamini kwamba kweli wazo la Cristiano Ronaldo ‘CR7’ kuondoka Real Madrid majira haya ya joto linaweza kutokea.

Baada ya taarifa hizo kuripotiwa katikati ya wiki, inadaiwa nyota huyo amewaambia wachezaji wenzake wa Ureno kwamba huo ndio msimamo wake na hakuna nafasi ya kubadili uamuzi huo tena.

Ronaldo amefikia uamuzi huo baada ya kukerwa na tuhuma za udanganyifu wa ukwepaji kodi Hispania kiasi cha Euro milioni 14.7.

Hivyo, wakati CR7 kukiwa na uwezekano wa kuondoka, klabu inayopewa nafasi kubwa kuunasa mtambo huo wa mabao ni Manchester United. Mbali ya yote, Ronaldo bado ni shujaa Old Trafford. Ronaldo mara zote amekuwa muwazi kuhusu kuipenda klabu yake hiyo ya zamani.

Huku Sir Alex Ferguson, Jorge Mendes [wakala wake] na kocha Jose Mourinho wote wakiwa na nguvu, hiyo inamaanisha kuna watu wa kutosha kumuunganisha na kurejea Old Trafford… kama watahitaji kufanya hivyo.

Hivyo, kurudi kwa Ronaldo United kwa ujumla kunaonekaje? Hapa kuna mawazo machache kuhusu kitakachotokea mapema mara baada ya kutua:

1. Bifu za Ronaldo, Mourinho
Kutakuwa na habari nyingi kuhusu bifu za Ronaldo-Mourinho wakati wakiwa Real Madrid.

Nyota hao wawili wa Ureno, tunaweza kusema kulikuwa na uhusiano wa kutatanisha wakati Mourinho akiinoa miamba hiyo ya Santiago Bernabeu, na katika matukio tufauti walikuwa wakitibuana, hizo ni habari zitakazokuwa zikikumbushiwa mara kwa mara.

2. Fergie atahusishwa haraka

Kocha Fergie mara moja atahusishwa katika mahusiano ya karibu na timu.

Hiyo ni kwa sababu ya asili ya uhusiano wa Ronaldo na Mourinho - na sehemu nyingine itakuwa ni kutokana na yeye kuchoshwa na kustafu kwake- na Ronaldo kurudi Old Trafford kutamfanya Sir Alex kufanya zaidi ya anavyoonekana tu amekaa jukwaani akitabasamu na kupeana mikono na watu maarufu [VIPs].

Sababu ni kwamba Fergie ni mtu pekee ambaye Ronaldo bado anamuita 'bosi'.

3. Wapinzani wakuu watahoji umri
Mashabiki wa Liverpool, Chelsea, Arsenal, Man City wote haraka wataanza kumshusha Ronaldo kutokana na kigezo cha umri.

"Ndiyo, sawa, hivyo United sasa imepata mmoja wa wachezaji wakubwa kwa kumrejesha kikosini. Na kweli amefunga zaidi ya mabao 40 kwa kila msimu.

"Lakini ana miaka 32, hana ubora kama aliokuwa nao hapo awali. Na ndiyo, hiyo inamaana bado ni bora kwa zaidi ya asilimia 99 ya wanasoka katika Premier League… lakini United bado inalipa fedha kubwa.

4. Ibrahimovic atasahaulika mepema
Ni wazi kazi nzuri ya Zlatan Ibrahimovic aliyoifanya Man United itasahaulika mapema.

Mabao aliyofunga Msweden huyo yatasahaulika mara moja na mashabiki wa Man United kutokana na kutua kwa mtambo huo wa mabao kutoka Real Madrid.

5. Griezmann hatatajwa tena
Jina la nyota wa Atletico Madrid, 'Antoine Griezmann' pia litatupiliwa mbali katika historia ya Man United na itabaki "Griezmann' ni nani?"

6. Mtukufu wa jezi namba 7
Jezi namba saba Man United itarejeshwa kwa ajili ya utukufu wake halali.

Ikumbukwe jezi namba saba United imevaliwa na mastaa kama George Best, Denis Law, Bryan Robson, Eric Cantona na David Beckham, kwa siku za hivi karibuni imekuwa kama pango kutokana na kumkosa mchezaji anayeitendea haki.

Baada ya Michael Owen, Angel Di Maria na Memphis Depay ambao wote walipewa na kuondoka, kurudi kwa Ronaldo kutamfanya kuonekana mmiliki bora wa jezi namba saba Man United tangu alipoondoka.

7. Rooney anaweza kubaki
Wayne Rooney na Ronaldo walikuwa 'mapacha' bora wakati wakicheza pamoja United, hivyo nyota huyo wa kimataifa wa England anaweza kufikiri kucheza pembeni kwa mshindi huyo wa kubobea wa Ballon d'Or kunaweza kumrejesha tena kwenye mafanikio.

8. Messi atachekelea kimya kimya
Lionel Messi atachekelea kimyakimya mwenyewe.

"Ukweli Ronaldo atafunga mabao machache kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na United - na hatayakaribia aliyofunga akiwa na Real Madrid. Na unajua hilo litakuwa na maana gani…

"Ukinara wa ufungaji utakuwa wangu! "Kila kitu changu!"

9. Mashabiki City watautaka usajili wa Messi
"Sasa tazama hapa, Pep. Tunajua ulikuwa unatusumbua tu hapo kabla kutokana na kuhusishwa na Messi. Lakini unajua kijana huyu unaweza kumpata katika masikio yake.

"Fanya hilo litokee… na haraka."

10. Mashabiki wa Arsenal watakasirika
"Kwa nini isiwe sisi kumsajili Ronaldo?", kwa nini hatumsajili staa yeyote?". "Arsene Wenger sajili staa!"
Powered by Blogger.