Tanzania, Malawi kwenye ishu ya Ziwa Nyasa tena...
SERIKALI imesema mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa mpaka
katika Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi yanatarajiwa kuanza tena
wakati wowote kuanzia sasa.
Hayo yalisemwa bungeni mjini hapa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Augustine Mahiga,
alipowasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka ujao wa
fedha.
Alisema mazungumzo hayo yatafanyika chini ya usuluhishi wa Rais Mstaafu
wa Msumbiji na Mwenyekiti wa Jukwaa la Viongozi na Wakuu wa Nchi
Wastaafu wa Umoja wa Afrika, Joaquim Chissano, akisaidiwa na Rais
Mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki.
”Wizara inasubiri kupata tarehe rasmi ya kuanza kwa mazungumzo hayo kutoka Ofisi ya Rais Mstaafu, Mheshimiwa Chissano," alisema.
Balozi Mahiga alisema mkutano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano
kati ya Tanzania na Malawi ulifanyika Lilongwe, Malawi Februari mwaka
huu.
Alisema kuwa katika mkutano huo, masuala mbalimbali ya ushirikiano
katika nyanja za kiuchumi, siasa, usalama, usafirishaji, nishati,
uendekezaji wa Bonde la Mto Songwe na biashara yalijadiliwa na
makubaliano kufikiwa.
Alisema Tanzania na Malawi zilitia saini mikataba miwili ya Huduma za
Anga na Mashauriano ya Kidiplomasia na kwamba mkutano huo ulizidi
kuimarisha uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Malawi.
Waziri huyo pia alilieleza Bunge jinsi Tanzania inavyonufaika na
uhusiano mzuri kati yake na nchi zingine zikiwamo Qatar, Kuwait,
Morocco, Irael Iran, China, India, Zambia, Kenya, Uganda, Ethiopia,
Afrika Kusini, Cuba, Czech, Finland, Uswisi, Canada, Uturuki, Japan,
Jamhuri ya Korea na Umoja wa Falme za Kiarabu.
MKATABA WA EPA
Balozi Mahiga pia alisema uchambuzi uliofanyika kuhusu Mkataba wa Ubia
wa Kiuchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Ulaya
(EAC-EU Economic Partinership Agreement - EPA) si rafiki kwa ustawi wa
Tanzania hasa katika utekelezaji wa azma ya serikali ya awamu ya tano ya
kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.
Alisema mkutano wa 18 wa Viongozi Wakuu wa Nchi za Afrika Mashariki
ulofanyika Dar es Salaam mwezi huu ulijadili suala hilo na kukubaliana
Rais wa Uganda ambaye ni Mwenyekiti wa jumuiya, kuongoza ujumbe kwenda
Umoja wa Ulaya kwa lengo la kutafuta mwafaka wa namna ya kuondoa
changamoto ya changamoto zilizopo katika mkataba huo.
Alisema ujumbe huo pia unalenga kuushawishi Umoja wa Ulaya kutoiadhibu Kenya wakati majadiliano ya kutafuta mwafaka yakiendelea.
Ili kutekeleza majukumu yake kwa mwaka ujao wa fedha, Balozi Mahiga
aliliomba Bunge kuidhinisha Sh. bilioni 150.845 kwa ajili ya bajeti ya
wizara yake. Kati yake, Sh. bilioni 142.845 ni za matumizi ya kawaida na
Sh. bilioni nane ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Balozi Mahiga pia alisema kuwa kati ya Sh. bilioni 142.845 zilizotengwa
kwa ajili ya matumizi ya kawaida, Sh. milioni 410 ni kwa ajili ya Mpango
wa Kujitathmini Kiutawala Bora Tanzania.
Katika mwaka wa fedha 2016/17, wizara hiyo iliidhinishiwa Sh. bilioni
162.109. Kati yake, Sh. bilioni 154.109 ni kwa ajili ya matumizi ya
kawaida na Sh. bilioni nane kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Mahiga alisema kuwa hadi, Aprili 30, mwaka huu, wizara yake ilikuwa
imepokea Sh. bilioni 95.038 sawa na asilimia 56 ya fedha zote
zilizoidhinishwa na Bunge. Kati yake, Sh. bilioni 83.039 ni kwa ajili ya
matumizi ya kawaida na Sh. bilioni 3.489 ni za miradi ya maendeleo.
No comments:
Post a Comment