Trending News>>

Taifa Stars kuweka kambi Misri, Mkude abaki

Kikosi cha wachezaji 20 wa timu ya mpira wa miguu ya Tanzania 'Taifa Stars' kinatarajiwa kuondoka kesho Jumanne saa 10.45 jioni kwenda Misri kufanya kambi ya siku nane kujindaa na mchezo dhidi ya Lesotho utakaofanyika Juni 10, 2017, Dar es Salaam.
Taifa Stars katika moja ya mechi zake, Taifa Dar es Salaam
Wachezaji hao 20 kutoka hapa Tanzania wataungana na wengine watatu ambao ni Nahodha Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Faridi Mussa wanaocheza ughaibuni katika kikosi hicho na kufanya jumla ya wachezaji kuwa 23 nchini Misri.
Nahodha Msaidizi, Jonas Mkude hatakuwepo kwenye msafara huo kutokana na ushauri wa madaktari walioelekeza kwamba nyota huyo wa Simba apate mapumziko ya angalau siku nne.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga ameridhia na kusema kuwa Mkude ataungana na wenzake Juni 8, mwaka huu timu itakaporejea kutoka Misri. Mayanga hajajaza nafasi ya Mkude.
Mchezo dhidi ya Lesotho ni muhimu kwa Tanzania ikiwa ni mechi ya kwanza kwa Taifa Stars katika Kundi 'L' kuwania nafasi muhimu ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2019 zitakazofanyika NCHINI Cameroon.
Mbali ya Lesotho na Tanzania, mataifa mengine katika Kundi 'L' ni Uganda na Cape Verde ambao pia wikiendi ya Juni 9, 10 na 11, mwaka huu watakuwa katika mchezo wa kwanza pia kuwania nafasi hiyo.
Kikosi cha Taifa Stars kinaundwa na makipa Aishi Manula  (Azam FC), Benno Kakolanya  (Yanga SC) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar).

Jonas Mkude akiwa hospitali akiendelea na matibabu baada ya kupata ajali ya gari jana Jumapili
Walinzi wa pembeni upande wa kulia ni Shomari Kapombe    (Azam FC) na Hassan Kessy (Yanga SC) wakati upande wa kushoto wapo Mohammed Hussein (Simba) na Haji Mwinyi  (Yanga SC).
Walinzi wa kati Erasto Nyoni  (Azam FC), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba SC) na Agrey Morris  (Azam FC) ilihali viungo wa kuzuia ni Himid Mao (Azam FC) na Jonas Mkude kutoka Simba SC ambaye hatasafiri na timu kwa sasa.
Viungo wa kushambulia Salum Abubakar (Azam FC), Said Ndemla  (Simba SC) na Mzamiru Yassin (Simba) wakati viungo wa pembeni ni Simon Msuva (Yanga SC), Shizza Kichuya (Simba SC) na Farid Mussa (Teneriffe, Hispania).
Washambuliaji wapo Mbwana Samatta (KRC Genk- Ubelgiji), Thomas Ulimwengu (AFC Eskilstuna – Sweden), Ibrahim Ajib (Simba SC), Mbaraka Yusufu (Kagera Sugar) na Abdurahman Mussa (Ruvu Shooting).
Timu hiyo iliingia kambini Machi 23, 2017 kwenye Hoteli ya Urban Rose, Dar es Salaam kabla ya kesho kwenda Misri na baadaye itarejea Tanzania kucheza na Lesotho, Juni 10, mwaka.

No comments:

Powered by Blogger.