Muhongo aenda kufungikia jimboni kwake
Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini na Mbunge wa Musoma Vijiji Prof.
Sospeter Muhongo amewasihi wakazi wa jimbo hilo kutokuingiwa na hofu
kufuatia uamuzi wa Rais Dkt Magufuli kumfuta kazi.
Prof. Muhongo amewataka wapigakura wake na rafiki zake kutokuwa na hofu kwani kwa pamoja watafanikiwa.
Kwa mujibu wa taarifa za ofisi yake, amewaahidi kutoa ushirikiano wa
kutosha kuhakikisha kuwa wanafikia malengo yao ya kimaendeleo kwa
kutimiza ahadi zake.
Taarifa hiyo ilitolewa na Katibu wa Mbunge huyo, Juma Ramadhan ambaye
alisema kuwa kilichotokea ni cha kawaida kwenye siasa na inawapasa
kusahau hayo ili waweze kusonga mbele katika kutekeleza miradi ya
maendeleo.
Kwa sasa tunajielekeza kujenga vyumba vya madarasa na miradi mingine ya
maendeleo, hivyo ni vyema tukaungana pamoja ili kuweza kutekeleza
majukumu haya, alisema msaidizi huo.
Wakazi wa jimbo hilo waliahidi kutoa ushirikiano kwa mbunge wao katika
kutekeleza miradi hiyo kwani yeye si kiongozi wa kwanza kuondolewa
kwenye wadhifa wake. Aidha, wakazi hao walisema kuwa kuondolewa kwa
Prof. Muhongo kuwe funzo kwa wateule wengine kuwa nafasi hizo si za
kudumu.
Mei 24 mwaka huu Rais Dkt Magufuli alimfuta kazi Waziri Muhongo kufuatia
kile alichosema ni kushindwa kusimamia kwa umakini sekta ya madini na
hivyo kupelekea serikali kupata hasara.
No comments:
Post a Comment