Trending News>>

Singida United yachekelea SportPesa Super Cup


Kocha msaidizi wa Singida United Fred Minziro amesema mashindano ya SportPesa Super Cup yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi kuanzia Juni 05 mwaka huu ni kipimo kizuri kwa timu yake kwa ajili ya maandalizi ya kuelekea katika msimu ujao wa ligi kuu.
Kocha msaidizi wa Singida United, Fred Minziro
Kocha Minziro amesema, mashindano hayo yatakuwa na ushindani mkubwa kutokana na kushirikisha timu kutoka Kenya, Zanzibar na Tanzania Bara ambapo ameongeza kuwa anaamini kikosi chake kitafanya vizuri kutokana na usajili uliofanyika.
"Haya mashindano ni makubwa lakini kwa upande wetu yamekuwa kama yakushtukiza lakini ni makubwa na yatakuwa na ushindani mkubwa na kwa upande wetu yatakuwa mazuri kwani yatasaidia kujua mwanzo tunapoanza na tunapoelekea katika Ligi," amesema Kocha Minziro.
Minziro amewataka Wanasingida kuona mambo mazuri katika mashindano ya SportPesa pamoja na Ligi Kuu Tanzania Bara kwa ujumla.
"Kwa ujumla Wanasingida wategemee mazuri kwasababu hata usajili wanausikia na tuangalie Jumatatu ambapo tutaanza kuingia katika hayo mashindano ndipo tutajua timu inaelekea wapi, " amesema Minziro.
Naye Katibu mkuu wa Singida United Abrahman Sima amesema, kikosi kipo kamili kwaajili ya mashindano hayo huku akiongeza kuwa mpaka sasa wameshawasajili wachezaji watano wa kimataifa na wanategemea kuwa na wachezaji saba kabla ya kuanza kwa Ligi kuu ya Soka Tanzania Bara msimu ujao.
"Nwapongeza SportPesa kwa kutupatia nafasi kama hii na timu ipo kambini. Tumeanza mazoezi jana rasmi na Wanasingida waamini timu yao itaanza vizuri japo vilabu tutakavyokutana navyo vimetoka kwenye Ligi lakini naamini aina ya wachezaji tuliokuwa nao tutafanya vizuri katika mashindano ya SportPesa, " amesema Abrahman Sima.
Sima amekanusha pia kuingia usajili na wachezaji wa ndani Deus Kaseke wa Yanga na Ibrahim Ajibu wa Simba SC ambapo ameongeza kuwa kwa sasa wachezaji wa kimataifa ni watano na lengo lao ni kuwa na wachezaji saba.
"Kwa wachezaji wa ndani mpaka sasa tuliofanya makubaliano nao ni Kenny Ally ambaye ataingia kesho, tuna Atupele Green na ameshawasili pamoja na Salum Chuku lakini hao wengine sio kweli lakini ikitokea wakawepo hapo baadaye tutawaambia, " amesema Sima.

No comments:

Powered by Blogger.