Kaimu Balozi wa Marekani Nchini Atembelea Wabia Mkoani Mwanza, Aangazia ushirikiano kati ya Watu wa Marekani na Watanzania
|
Mwanza, TANZANIA. Tarehe 3 Mei, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania
na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Virginia Blaser alifanya ziara ya siku
moja kuwatembelea wabia mbalimbali mkoani Mwanza kuona shughuli zao akiangazia
ushirikiano imara uliopo kati ya watu wa Marekani na Watanzania katika sekta
mbalimbali.
Kaimu Balozi Blaser alianza ziara yake kwa kushiriki katika maadhimisho
ya Siku ya Uhuru wa Habari ambayo kwa miaka miwili iliyopita Ubalozi wa
Marekani umekuwa ukiyafadhili. “ Uhuru wa habari ni muhimu sana katika jamii ya
kidemokrasia inayolinda haki za watu,” alisema Kaimu Balozi Blaser katika
hotuba yake katika maadhimisho hayo. Aidha, alisisitizia umuhimu wa waandishi
wa habari na wadau wengine wa vyombo vya habari kushirikiana kwa kuchangia
mawazo na kusaidiana kama sehemu ya mtandao mkubwa wa kimataifa unaotoa na
kuelezea mitazamo mbalimbali na kuwapa raia sauti kuelezea kero na dukuduku zao.
Katika
ziara yake katika Taasisi ya Mafunzo ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Pasiansi,
ambayo inatoa mafunzo ya uhifadhi wa wanyamapori na kukabiliana na ujangili kwa
askari wa wanyamapori wa Kitanzania, Kaimu Balozi Blaser alishuhudia wanafunzi
wakionyesha kwa vitendo ujuzi walioupata katika usimamizi wa sheria, mbinu za
medani na historia ya viumbe asilia. Serikali
ya Marekani iliichangia taasisi ya Pasiansi kwa kufadhili mafunzo kwa
wafanyakazi wake nane ili kusaidia kujenga uwezo wa kulinda wanyamapori nchini
Tanzania.
Hali kadhalika, Kaimu Balozi Blaser alipata fursa ya kushuhudia matokeo
chanya ya msaada wa Serikali ya Marekani katika nyanja ya usalama pale
alipotembelea Chuo cha Polisi Wanamaji cha Mwanza na kuona doria ya majini
inayofanywa na askari hao kwa kutumia boti maalumu ya doria (Defender Boat)
ilitolewa na Marekani chini ya Mpango wake wa Ubia na nchi za Afrika katika
kulinda Amani (African Partnership for Rapid Response Peacekeeping). Mbali na boti mbili zilizotolewa kwa Chuo cha
Polisi Wanamaji, Marekani ilitoa boti nyingine nane kwa Tanzania na kuwezesha
matunzo na matengenezo yake.
Katika sekta ya afya, Kaimu Balozi Blaser alizungumza na watoa huduma
zinazohusu matibabu na kinga dhidi ya VVU/UKIMWI kwa jamii wa kujitolea (Community
Outreach Volunteers) ambao wamekuwa wakitoa elimu na huduma za kujikinga na VVU
kwa makundi-rika yao chini ya mpango wa ICAP unaoendeshwa na Chuo Kikuu cha
Columbia. Mpango huo ni wabia wa Taasisi ya Marekani ya Kudhibiti Maradhi (CDC)
na Mpango wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI. Aidha alikutana na wafanyakazi wa kujitolea wa
Kimarekani kutoka Peace Corps wanaofanya kazi katika hospitali ya Bugando
wakisaidia kuimarisha utoaji wa elimu kwa matabibu na wauguzi na kuimarisha
taratibu za utoaji matibabu. Akiwa
katika Kituo Maalumu cha Matibabu ya UKIMWI kwa watoto kiitwacho Baylor
International Pediatric AIDS Initiative HIV Care Center of Excellence – kilichojengwa
kwa ubia kati ya Serikali ya Marekani na Sekta binafsi nchini Marekani na
kupata msaada wa wataalamu na uendeshaji wake kupitia Shirika la Marekani la
Ushirikiano wa Kimataifa (USAID) –
Kaimu Balozi Blaseraliwashukuru wafanyakazi wa kituo hicho kwa kutoa
matunzo na matibabu kwa watoto waliopata maambukizo ya VVU na kuchangia katika
jitihada za kufikia lengo la Umoja wa Mataifa la 90-90-90 yaani kuhakikisha
asilimia asilimia 90 ya
walioathirika na maambukizi ya VVU wanapimwa na kujua hali zao kiafya, asilimia
90 ya watakaopimwa na kukutwa na VVU wanapata dawa za kufubaza VVU na asilimia 90 ya waliopo kwenye tiba
wawe wameweza kuvidhibiti virusi hivyo kwa kiwango kikubwa.
No comments:
Post a Comment