Trending News>>

CHAMA Cha Wanyakazi wastaafu wilaya ya Singida kimesema kuwa idadi kubwa ya wafanyakazi waliostaafu utumishi wa serikali hawajui kuwa  wanapaswa kulipwa mafao kwa kipindi cha miaka mitatu mara baada ya mume au mke wa mnufaika wa mafao hayo atakapofariki.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyakazi Wastaafu Mkoa wa Singida,Shabani Mwanja aliyasema hayo kwenye mkutano wa wanachama wa chama hicho uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo cha walimu Nyerere,Manispaa ya Singida.
Alifafanua Mwanja kwamba  iwapo mtumishi wa serikali aliyestaafu anapokea mafao ya uzeeni,endapo atafariki mwenza wake atapaswa kulipwa mafao hayo( Survival Penshen) kwa kipindi cha miezi 36 (miaka mitatu) yeye pamoja na mtoto ambaye alikuwa bado tegemezi wa marehemu.
“Watumishi wale wanaopokea pensheni serikalini akifariki mwenza wake analipwa survaival Penshen miezi 36 au miaka mitatu yeye na mtoto wake ambaye alikuwa bado tegemezi wa marehemu,mnanielewa hapo ?”alihoji Makamu Mwenyekiti huyo.
Aidha Mwanja alibainisha pia kuwa kama mama amefariki wakati alikuwa akipokea malipo ya pensheni,baba atalipwa miezi 36 na mtoto tegemezi ambaye alikuwa bado ana umri mdogo,au mama vile vile atalipwa kwa ajili ya mume wake aliyefariki akiwa analipwa pensheni na mtoto ambaye alikuwa tegemezi.
“Hiyo mlikuwa mnaielewa sasa ikitokea nenda kwenye mfuko unaohusika utalipwa Survaival Penshen,sawa eeeh ?”aliwahoji wanachama hao wa wafanyakazi wastaafu.
Kwa upande wake Katibu wa Chama hicho Wilaya ya Singida,Hassani  Dumwala aliweka bayana kwamba lengo la kuanzishwa kwa chama hicho ni kupigania maslahi ya wafanyakazi wastaafu ili waweze kunufaika na huduma wanazotakiwa kupatiwa na serikali baada ya utumishi wao kufikia ukomo.
Aidha Katibu Dumwala alizitaja baadhi ya haki ambazo wanachama wao hawanufaiki kwa mujibu wa sheria kuwa ni huduma duni za matibabu,malipo pensheni ya shilingi laki moja yaliyopitwa na wakati, haitoshelezi chochote kile kwa wakati uliopo kwa sasa.
Kwa mujibu wa Katibu huyo kwa kuwa serikali inawaamini wastaafu hao na kikubwa zaidi kwa kuwa ilishawaona utendaji wao wa kazi,hivyo alitumia fursa hiyo kuiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwaongeza malipo yao ya mafao ya pensheni,ili yaweze kuwasaidia kujikimu kimaisha,kwani kiwango wanacholipwa kwa sasa ni kidogo huku hali ya maisha ikizidi kupanda.
Katibu huyo wa Chama Cha Wafanyakazi wastaafu wilaya ya Singida hata hivyo aliwahakikishia wanachama hao kwamba wanaandaa utaratibu wa kuwaita watendaji wa mifuko ya hifadhi ili wakatoe elimu juu ya haki za wastaafu hao kwa kila mfuko uliosajili wanachama hao.
Akifunga mkutano huo wa wafanyakazi waliostaafu kwa niaba ya Ofisa Tarafa ya Unyakumi,Edward Salumu alitumia fursa hiyo kuwahimiza wanachama hao kutokosa kuhudhuria kwenye mkutano wao unaotarajia kufanyika jan,31,mwaka huu kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo cha Walimu Nyerere,Manispaa ya Singida lengo likiwa kupata viongozi.
Mkutano huo wa wanachama wa wafanyakazi waliostaafu wilaya ya Singida ulilazimika kutofanyika na hivyo kuahirishwa hadi jan,31,mwaka huu baada ya wanachama kutoka katika kata za Mwankoko,Utemini,Uhamaka na Mandewa kutohudhuria kwenye mkutano huo. 

Baadhi ya wanachama wa chama cha wafanyakazi wastaafu wa wilaya ya Singida wakiwa kwenye ukumbi wa mikutano wa kituo cha walimu Nyerere,Manispaa ya Singida wakiwa na lengo la kuchagua viongozi wao.



 Baadhi ya wanachama wa chama cha wafanyakazi wastaafu wa wilaya ya Singida wakipiga kura za kukubaliana kuahirishwa kwa mkutano huo baada ya wajumbe wa kata nne kutohudhuria kwenye mkutano huo na nhivyo kupangwa kufanyika tena jan,31,mwaka huu.(Picha zote na Jumbe Ismailly)

No comments:

Powered by Blogger.