Trending News>>

Kikosi kazi cha kulinda watoto mitandaoni chaja


SHIRIKA lisilo la Kiserikali la C-Sema kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wameandaa kikosi kazi kwa ajili ya ulinzi wa watoto mitandaoni, lengo likiwa ni kuhakikisha wanadhibiti matumizi ya picha mbaya za ukatili dhidi ya watoto.

Mtendaji Mkuu wa C-Sema, Kiiya Joel alisema jana kuwa kikosi hicho, kina mitandao yote ya simu ili kuangalia na kuhakikisha mtoto wa kitanzania anakuwa katika mazingira mazuri na salama.

“Tumeshafanya vikao vitatu na lengo kubwa ni kuwa na mfumo mzuri ili ukiona kuna video inatembea kwenye mitandao au picha uwe na mahali pa kuipeleka au kusemea… lengo ni kutengeneza mfumo mzuri wa ulinzi ili baada ya kuiripoti video au picha inayosambaa itolewe,” alisema.

Pia alisema kikosi kazi hicho kinahakikisha video na televisheni zinazoangaliwa majumbani, zinakuwa na vipindi vyenye maadili na maudhui kwa watoto, kwa kuwa kwa sasa kuna vipindi ambavyo havina maudhui kwa watoto, hivyo wataangalia ni vitu gani vinafaa kuangaliwa kwa mazingira ya mtoto wa kitanzania na kuhakikisha wanachokiona kinaendana na umri wao na maadili yao.

“Wazo la kuanzisha kikosi hiki lilikuja Mei 2015 ambapo TCRA walitupa fursa ya kwenda Geneva kujifunza sisi kama watoaji wa huduma ya simu kwa mtoto, pia tulienda na maofisa wa TCRA, hivyo tulijifunza nini wenzetu wanafanya na tunayafanyia kazi,” alieleza.

Alisema baada ya hapo, mkutano wa kwanza ulifanyika mwanzoni mwa mwaka huu na wakaamua kuanzisha kikosi kazi, ambacho kinajumuisha polisi, wizara zote zinazohusika na masuala ya watoto, wadau mbalimbali katika idara za watoto, makampuni ya simu na yale yanayotoa huduma ya intaneti.

Alisema baada ya kikosi kazi kuanzishwa, tayari kimefanyiwa mafunzo na Umoja wa Mitandao ya Simu Duniani ambao makao makuu yake yapo Uingereza, hivyo wana timu yenye uelewa mpana kuhusu ulinzi wa mtoto mitandaoni.

“Kumekuwepo na picha nyingi na video zinazoonesha ukatili wanaofanyiwa watoto kwenye mitandao… hili halifai kufumbiwa macho hivyo kikosi hicho kitakuwa kikihakikisha mambo kama hayo yanadhibitiwa na mtoto anakuwa salama,” alieleza.

No comments:

Powered by Blogger.