Biashara Tano Unazoweza Kuanza Kufanya Mwaka 2017 Kwa Mtaji Kidogo Au Bila Ya Mtaji Kabisa
Popote ambapo utaanza kuzungumza kuhusu biashara, wale ambao hawajaanza biashara watakuambia kitu kimoja; napenda kuanza biashara lakini sina mtaji. Hii ni sababu ya uongo ya kushindwa kuingia kwenye biashara ambayo imekuwa inatumiwa na watu wengi ambao hawapo tayari kuingia kwenye biashara.
Yaani mimi ninachoamini ni hiki, mtu anaponiambia kwamba anashindwa kuingia kwenye biashara kwa sababu hana mtaji, ninachoelewa ni kwamba mtu huyu hayupo tayari kujitoa na kuingia kwenye biashara. Ila anaona aibu kukubali hilo na hivyo anatafuta sababu ya uongo.
Nasema hivi kwa sababu dunia ya sasa zipo fursa nyingi za kuanza biashara hata kama huna mtaji kabisa. Zipo biashara nyingi ambazo mtu anaweza kuzianza bure kabisa na zipo nyingine mtu anaweza kuanza na mtaji kidogo.
Kitu kingine kikubwa ambacho kinanishawishi wanaosema hawana mtaji wa biashara wanaficha uzembe wao ni sababu hiyo kutokuwa na ukomo. Yaani unakuta mtu kila mwaka anatumia sababu hiyo hiyo kwamba hana mtaji. Sasa unajiuliza mwisho wa sababu hii ni lini?
Kama unavyojua rafiki yangu, mwaka 2017 sitaki utani kabisa na wewe, kama umeamua kubadili maisha yako basi lazima ukafanye kitu kwa mwaka huo. Na kitu cha kwanza kabisa ambacho nimekuambia ufanye ni kuacha kabisa kuweka malengo kwa mwaka huo 2017. Badala yake nitakupa mfumo mpya wa kuendesha maisha ambao siyo wa malengo, mfumo huo ni bora kuliko malengo. Kujifunza haya yote karibu kwenye semina ya mwaka 2017 ambayo itaanza tarehe 04/01/2017 kwa njia ya mtandao. Kupata taarifa zaidi za semina hii bonyeza maandishi haya.
Mwaka 2017 siyo mwaka wa sababu au visingizio, ni mwaka wa kufanya. Na moja ya vitu ambavyo nimekuambia ufanye ni kuanza au kukuza biashara yako. Sasa kwa kuwa bado utatumia ule uzembe wako wa zamani wa kusema SINA MTAJI, leo hapa nakushirikisha biashara tano unazoweza kuanza kufanya kwa mtaji kidogo au bila ya mtaji kabisa.
1. Toa huduma.
Kama huna mtaji wa fedha, basi nina uhakika una mtaji wa muda. Sasa tumia muda wako kutoa huduma ambayo wengine wanaihitaji. Toa huduma kulingana na utaalamu wako, uzoefu wako au ujuzi ulionao. Angalia ni namna gani unaweza kutumia muda wako kuongeza thamani zaidi kwenye maisha ya wengine.
Kwa mfano kama wewe ni mwalimu, basi unaweza kutenga muda wako wa ziada kutoa huduma ya kufundisha watoto shuleni au hata majumbani mwao. Kama wewe unaweza kufanya kitu fulani, basi tafuta wenye uhitaji wa kitu hiko na wasaidie kwa muda ulionao. Unaweza kuwasaidia watu kwa kazi zao za nguvu au hata kazi zao za kitaalamu. Unaweza kuwasaidia watu wanaofanya tafiti mbalimbali kwa muda wako na utaalamu wako kwenye tafiti.
Kikubwa zaidi unaweza kutoa huduma ya ushauri kulingana na ujuzi na hata uzoefu ulionao kwenye maeneo mbalimbali. Iwe ni kilimo, biashara, afya na kadhalika.
2. Biashara ya mtandao (network marketing).
Najua wengi mkisikia hii huwa mnakunja sura na kuona kama mnapotezwa. Bado naendelea kusisitiza kama unataka kuigia kwenye biashara na hujui wapi uanzie, basi ingia kwenye biashara ya mtandao. Hii ni biashara ambapo unatumia bidhaa au huduma fulani, kisha unawashawishi wengine nao watumie na unalipwa kamisheni kwa manunuzi wanayofanya.
Ni biashara nzuri kuingia kama hujawahi kufanya biashara kabisa na hujui wapi uanzie. Kwenye biashara hizi unafundishwa mengi na nyingi unaweza kuingia kwa mtaji kidogo wa chini ya shilingi laki moja.
3. Biashara ya taarifa na maarifa.
Unaweza kuingia kwenye biashara ya kutoa taarifa na maarifa. Kwa dunia ya sasa ambapo watu wengi wanatumia mtandao wa intaneti, unaweza kutumia mtandao huu kutoa taarifa na maarifa na kuweza kutengeneza kipato.
Unaweza kufanya hivi kwa kuanzisha blog ambayo utaitumia kutoa taarifa na maarifa fulani ambayo wewe unayo, kwa ujuzi au uzoefu. Baadaye unaitumia blog hii kutengeneza kipato kwa kupitia matangazo na hata kuuza bidhaa na huduma zako nyingine.
Pia unaweza kutoa taarifa na maarifa kwa njia ya uandishi wa vitabu. Unaweza kuandika vitabu na kuuza kwa nakala tete (softcopy) kama huna mtaji wa kuvichapa.
4. Kilimo biashara.
Kuna fursa kubwa sana kwenye kilimo cha kibiashara, hasa kwa kilimo cha muda mfupi cha mboga mboga na matunda. Kilimo hiki unaweza kuingia kwa mtaji kidogo na kama una muda wa kutosha kukifuatilia kwa makini basi unaweza kuanza kidogo na kukua kadiri muda unavyokwenda. Angalia kilimo kipi unaweza kuanza nacho na ukaribu wako ili uweze kupata matokeo mazuri.
5. Biashara yoyote unayotaka kuanza, ila anza kidogo.
Unaweza kuanza biashara yoyote unayopenda kuanza, hata kama ina uhitaji wa mtaji mkubwa, wewe anza kidogo. Anza kwa hatua ya chini kabisa, weka juhudi kubwa na endelea kuikuza.
Ukishaanza kuona matokeo mazuri, yaani faida kwa hatua hiyo ndogo unayopiga, ni rahisi kuwakaribisha watu wengine na wakakuchangia mtaji. Au hata kwenda kwenye taasisi za kifedha na kuchukua mkopo.
Wapo watu ambao wamekuwa wanafikiri kama wakipewa mkopo basi wataanzisha biashara, tatizo siyo mkopo, tatizo ni wewe kutojua biashara, ndiyo maana hakuna mtu mwenye akili zake timamu atakayekupa wewe mkopo wa kwenda kuanza biashara, kama hujawahi kufanya biashara kabisa. Kwa sababu anajua anakusindikiza kwenda kupata hasara. Anza biashara kidogo na ukishaanza kupata faida unaweza kuwashawishi watu wakupe mtaji zaidi.
Rafiki kama nilivyokuambia, mwaka huu 2017 sitaki uupoteze kama ambavyo umepoteza miaka mingine ya nyuma. Nataka ufanye kitu mwaka huu, ambacho kitaleta mabadiliko makubwa kwenye maisha yako. Anza kufanya sasa na nakuhakikishia tupo pamoja kwenye safari hii.
No comments:
Post a Comment