Trending News>>

Tisa kizimbani kwa uwindaji haramu


Mbeya.
 Watu tisa wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mkoa jijini hapa wakikabiliwa na kesi mbili tofauti za uhujumu uchumi kupitia uwindaji haramu wa wanyamapori.

Katika kesi hizo walizosomewa jana, shauri la kwanza linawakabili Fahad Haroon Pirmohamed, Pirmohamed Abdullack Mulla wakazi wa Mbarali, Shahad Nawab Mulla na Shahgol Majid Mulla wakazi wa Mkoa wa Njombe pamoja na Mikidadi Mwazembe ambaye ni mkazi wa Kongoro Mswiswi wilayani Mbarali.

Mshtakiwa Pirmohamed Mulla alipanda kizimbani kwa mara ya pili katika kipindi cha miezi miwili baada ya awali kufikishwa katika Mahakama hiyo kwa mashtaka ya kumiliki nyara mbalimbali za Serikali.

Katika kesi hiyo alikiri kosa na kuhukumiwa kwenda jela miaka 20 au kulipa faini ya Sh138,390,000 ambazo alilipa na kupata risiti ya Serikali yenye namba 8870022.

Jana, waendesha mashtaka wa Serikali, Basil Namkambe na Habel Kihaka walidai kuwa washtakiwa kwa pamoja walitenda kosa la kuwinda na kuua wanyamapori waliokatazwa.

Kihaka alidai washtakiwa hao walitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti kati ya Agosti 2006 na Septemba 2014 kwenye maeneo ya mikoa ya Mbeya, Iringa, Tanga na Morogoro.


Pia, katika kipindi hicho washtakiwa hao wanadaiwa waliwinda kisha kuwaua tembo 86 na nyati watano wote kwa pamoja wakiwa na thamani ya Sh2.8 bilioni mali ya Serikali kinyume na sheria za wanyamapori.

Waendesha mashtaka walidai katika kipindi hicho washtakiwa hap waliua pofu wawili, parahara wawili, swalapara wawili na kongoni watano wote wakiwa na thamani ya Sh30 milioni.

Katika kesi ya pili inayowakabili Mazar Gamdust, Abdulsamad Abdallah, Juma Msagati na Sylevester Lugola wote wakazi wa wilayani Mbarali, kwa pamoja na nyakati tofauti kati ya Januari 2000 na Septemba 2014, kwenye mikoa ya Mbeya na Iringa waliwinda na kuwaua wanyama waliokatazwa huku wakiwa hawana kibali cha kufanya hivyo kinyume na sheria za wanyamapori.

Pia, Namkambe alidai wanashtakiwa hao waliwaua wanyama waliokatazwa kisheria huku wakiwa hawana kibali.

Aliwataja viumbe waliouawa kuwa ni tandala wadogo sita, pofu watatu, njiwapori watatu, swala para wawili na kongoni saba wote wakiwa na thamani ya Sh54 milioni. Washtakiwa wote kupitia kwa mawakili wanaowatetea Yusuph Mohamed na Jovin Ndungi walikana mashtaka hayo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Machael Mteite aliamuru washtakiwa wote kurudishwa rumande hadi Novemba 17 siku ambayo kesi ya kwanza itasikilizwa na ile ya pili hadi Novemba 24 shauri lao litakapotajwa tena.

No comments:

Powered by Blogger.