Trending News>>

Nyavu haramu za zaidi ya Sh7 bilioni zawapandisha kizimbani


Dar es Salaam. Raia wa China Fu Chang Feng, mtanzania, Jeremiah Kerenge na raia wa India, Ally Raza wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu likiwamo la kuagiza nyavu haramu za kuvulia samaki aina ya Monofilament zenye thamani ya zaidi ya  Sh7.4 bilioni zilizopigwa marufuku hapa nchini kuhifadhiwa wala kutumika.

Akisoma hati ya mashtaka leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenye alidai kuwa washtakiwa Fu Chang na Kerenge , Oktoba 4,2016 huko Kurasini Shimo la Udongo walifanya kosa la uhujumu uchumi.

Alidai kuwa siku hiyo washtakiwa hao  wakiwa kwenye eneo hilo lililopo wilaya ya Ilala na Temeke waliagiza  kontena lenye namba TCNU 9551946 kutoka Shanghai, China  kwenda  Tanzania  lililokuwa limebeba nyavu haramu ambazo haziruhusiwi hapa nchini kuvulia Samaki 499 aina ya Monofilament zenye thamani ya Sh7.485 bilioni.

Wakili huyo wa Serikali, Kishenyi amedai kuwa Oktoba 5,2016 katika Mtaa wa Ilala Mafuriko,  washtakiwa   Feng (50), Kerenge(40) na Ally Raza (34) kwa pamoja walikamatwa wakiwa wamehifadhi mifuko 35 iliyokuwa imebeba nyavu hizo haramu 187 aina ya Monofilament zenye thamani ya Sh 15.193 bilioni ambazo zilikuwa zimepigwa marufuku hapa nchini kuhifadhiwa wala kutumika.

Iliendelea kudaiwa mahakamani hapo kuwa Oktoba 5,2016 katika mtaa wa Mafuriko  Ilala, washtakiwa hao walikamatwa wakiwa wamehifadhi mifuko 50 iliyobeba nyavu haramu 200 ndogo chini ya inchi 3 aina ya Gillnet zenye thamani ya Sh300 milioni ambazo zilimepigwa marufuku kuhifadhiwa ama kutumika.

Washtakiwa hawakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi hadi Mahakama Kuu.

Hata hivyo wakati kesi hiyo ikiendelea raia wa China amesomewa mashtaka yanaomkabili kupitia mkalimani, upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Baada ya washtakiwa kusomewa mashtaka hayo, Wakili wa Kujitegemea, Roman Lamwai ameomba mahakama impatie dhamana mteja wake Ally Radha kwa sababu mashtaka yanayomkabili hayapo chini ya sheria ya uhujumu uchumi.

Wakili Mutalemwa yeye amedai kuwa hiyo kesi ni ya uhujumu uchumi ndio maana washtakiwa hawakuruhusiwa kuongea chochote na akashauri hoja za dhamana zielekezwe Mahakama Kuu.

Baada ya kutolewa kwa hoja hizo, Hakimu Mwambapa amesema atatoa uamuzi kama mshtakiwa huyo atapa dhamana ama la kesho saa nne asubuhi.

No comments:

Powered by Blogger.