Trending News>>

Wachezaji 10 wakali kwenye Kombe la Dunia Russia-2018



Lionel Messi wa Argentina katika mechi na timu yake ya Barcelona, January 2018. / AFP PHOTO / LLUIS GÈNE

Lionel Messi, Argentina


Nyota huyu wa Argentina haitaji “kombe” la dunia kuthibitisha ubora wake katika kandanda duniani. Magoli aliyofunga, ubingwa kadha wa La Liga, ubingwa wa champions league, rekodi alizoweka, tuzo kadha na chenga zinazoziba pumzi ni ushahidi tosha wa uhodari wake katika kandanda kwa zaidi ya miaka kumi sasa.

Hata hivyo, kuna kitu kinakosekana. Hajawahi kuishindia nchi yake kombe katika mashindano makubwa kama vile fainali za Kombe la Dunia au Copa America. Katika Kombe la Dunia ameishia kwenye robo fainali mara mbili, na mwaka 2014 timu yake ikaanguka katika mechi ya mwisho dhidi ya Ujerumani waliochukua ubingwa. Pele aliipatia Brazil Kombe la Dunia mara tatu, Diego Maradona aliipatia Argentina kombe hilo mara moja. Je wakati wa Messi umefika?

Cristiano Ronaldo, Ureno

Kama Messi ni mchezaji bora kuliko wote duniani basi Cristiano Ronaldo hayuko mbali sana nyuma yake. Mashabiki wa kandanda duniani lazima wakubali bahati waliyo nayo kuona wachezaji wawili bora kama Messi na Ronaldo wakishindana mara kadha katika kila msimu wa ligi za Spain. Wakati Messi anastarehesha kwa chenga zake jinsi anavyozungusha walinzi, Ronaldo anatumia spidi, nguvu na uhodari wa kuruka kuliko wachezaji wengi katika msitari wa ushambuliaji. Ameshinda ubingwa wa La Liga mara nne kati ya miaka mitano iliyopita. Aliisaidia Ureno kushinda ubingwa wa Ulaya mwaka 2016, lakini katika Kombe la Dunia tangu aingie timu ya taifa 2006 ameishia tu katika nafasi ya nne.

Neymar, Brazil

Mwaka 2014 matumaini ya Brazil kushinda Kombe la Dunia nyumbani yalitoweka baada ya Neymar kuumia mgongo katika robo fainali. Hivi sasa wasiwasi upo katika mguu wake. Amepona vya kutosha baada ya kuumia Februari akicheza mechi na timu yake ya Paris Saint-Germain. Lakini bila ya kuwa katika mechi zenye upinzani mkubwa kabla ya Kombe la Dunia, Neymar anahitaji kujirudisha katika ubora wake haraka sana. Brazil imeunda kikosi kizuri sana na endapo Neymar atakuwa katika ubora wake basi Brazil ina nafasi nzuri ya kushinda kombe hilo.

Mohamed Salah, Misri

Kwa kawaida katika mashindano makubwa kama Kombe la Dunia wachezaji bora mara nyingi wanatokea Ulaya na Amerika Kusini – na mara moja moja Afrika Magharibi. Hawatokei Afrika Kaskazini, lakini sasa? Katika msimu wake huu na klabu ya Liverpool Mo Salah aliweka rekodi ya kufunga magoli mengi (32) katika ligi ya Uingereza kwa msimu. Alifunga magoli mengine 12 katika mashindano ambayo si ya ligi – kiwango cha kushangaza kwa mchezaji ambaye hakupata nafasi ya kucheza sana alipokuwa Chelsea kutoka mwaka 2013 hadi 2015. Akiwa Roma alikuwa na mafanikio lakini si kama alivyofanya na Liverpool msimu huu kuiongoza hadi fainali ya Champions League. Baada ya kuumia bega katika mechi ya fainali baina ya Liverpool and Real Madrid kulikuwa na wasiwasi kama Mo Salah ataweza kurudi katika timu ya taifa ya Misri na kucheza mechi ya kwanza na Uruguay Juni 15 - siku ambayo Mo Salah atatimiza miaka 26.

David de Gea, Hispania

Katika kandanda walinda mlango kwa kawaida wanafikia kiwango cha juu kabisa kadri umri wao unavyokwenda juu. Akiwa na umri wa miaka 27 tu, de Gea ndio kwanza anaanza lakini amejikuta tayari katika kiwango cha pekee langoni. De Gea alikuwa golikipa bora katika ligi ya Uingereza msimu huu na huenda Ulaya nzima. Mashabiki wa Manchester United walimchagua kama mchezaji bora wa msimu akiwa amerekodi mechi 18 kati ya 37 bila kufungwa goli. Anacheza na timu nzuri ya Hispania katika mashindano haya ambapo ubora wake bila shaka utaonekana zaidi. Na baada ya misimu saba pale Old Trafford, de Gea huenda akavutwa na Real Madrid baada ya Kombe la Dunia.

Eden Hazard, Ubelgiji

Kwa spidi ya ajabu miguuni mwake na jinsi anavyouona uwanja winga huyu wa Ubelgiji anafananishwa na Lionel Messi mara nyingine. Uwezo wake wa kupasua njia kati ya walinzi anafanya mtu ategemee chochote kinaweza kutokea mpira unapokuwa mguuni mwa Eden Hazard. Tangu ajiunge na Chelsea kutoka Lille, Ufaransa mwaka 2012, Hazard amefunga mabao 89 katika mashindano kadha na kushinda tuzo ya mchezaji wa mwaka wa klabu hiyo mara tatu. Katika michuano ya awali ya kombe la dunia, Hazard alifunga magoli sita katika mechi nane.

Antoine Griezmann, Ufaransa

Wakati nyota wengi wa Kombe la Dunia wanatokea klabu maarufu kama vile Real Madrid, Barcelona na Manchester United, Griezmann anatokea klabu yenye historia kubwa - Atletico Madrid – lakini mafanikio madogo katika La Liga. Griezmann amepata mafanikio ya wastani wa magoli 20 katika misimu mine na timu hiyo tangu ahamie hapo kutoka Real Sociedad. Alijunga na timu ya taifa ya Ufaransa mwaka 2014 akiwa na umri wa miaka 23. Miezi mitatu baadaye alichukua namba ya timu ya kwanza katika Kombe la Dunia la 2014.

James Rodriguez, Colombia

Sifa zake ziliibukia katika Kombe la Dunia 2014 ambapo mashabiki wa Brazil walimkubali vizuri mshambuliaji huyo wa Colombia. Uchezaji wake katika mashindano hayo ulimpatia uhamisho wa nguvu hadi Real Madrid lakini baada ya msimu wa kwanza wenye mafanikio, alijikuta akipambana sana kupata namba katika timu hiyo. Msimu huu uliopita Rodriguez alikuwa Bayern Munich kwa mkopo na kufunga magoli saba katika Bundesliga.

Thomas Mueller, Ujerumani

Ingawaje idadi yake ya magoli na timu ya Bayern Munich imepungua katika misimu miwili iliyopita, mshambuliaji huyu sio wa kumpuuza hata kidogo katika mashindano ya kimataifa. Akiwa uwanjani Mueller hatishi sana kama Messi au Ronaldo lakini anajua tu kuweka mpira kimiani. Alifunga magoli matano katika Kombe la Dunia la 2010 Afrika Kusini na matano mengine Brazil 2014. Kwa magoli 10 katika Kombe la Dunia Mueller ni mmoja wa wachezaji wenye magoli mengi katika historia ya mashindano hayo..

Gabriel Jesus, Brazil

Unatafuta mchezaji atakeibuka nyota Russia 2018. Muangalie Gabriel Jesus wa Brazil. Miaka minne iliyopita kijana huyu wa miaka 21 ambaye sasa ni mshambuliaji wa Manchester City alikuwa anachora picha za Kombe la Dunia katika mitaa ya Sao Paulo. Katika msimu wake wa pili Uingereza Jesus amefunga magoli 13 katika mechi 29 za premier league na magoli manne katika champions league. Huenda akawa katika 11 ya kwanza ya Brazil mbele ya Roberto Firmino wa Liverpool timu hiyo wa Wana Samba itakapoingia uwanjani katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Uswisi.

No comments:

Powered by Blogger.