Rekodi ambayo haitavunjwa kwenye Kombe la Dunia
Kuelekea fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 zinazoanza Alhamisi hii Juni 14 nchini Urusi, kuna rekodi mbalimbali ambazo zinaweza kuvunjwa lakini rekodi ya Pele itaendelea kusimama.
Rekodi ya nyota huyo wa Brazil Edson Arantes do Nascimento maarufu kama Pele, ya kutwaa Kombe la Dunia mara tatu itaendelea kusimama kutokana na wachezaji 736 wa timu 32 zinazoshiriki fainali za mwaka huu kutokuwepo hata mmoja ambaye ameshatwaa mara mbili.
Pele alitwaa Kombe lake la kwanza mwaka 1958, akiwa na umri wa miaka 17 ambapo alifanikiwa kufunga mabao 6 kwenye fainali hizo, yakiwemo mabao mawili kwenye mchezo wa fainali dhidi ya wenyeji Sweden.
Nyota huyo ambaye anatajwa kuwa ndio mchezaji bora wa soka wa muda wote, alifanikiwa kuchukua Kombe la pili kwenye fainali zilizofanyika nchini Chile mwaka 1962. Hata hivyo Pele hakucheza kwa kiwango kikubwa kwenye fainali hizo kutokana na kupata majeraha.
Alihitimisha mafanikio yake kwa kuchukua Kombe kwenye fainali za mwaka 1970 nchini Mexico. Katika fainali za mwaka huu kuna wachezaji waliochukua mara moja tu, kama Andres Iniesta, Sergio Ramos, Sergio Busquet, Mesut Ozil, Tony Kroos, Thomas Muller, Manuel Neuer, Iker Casillas na wengine wachache kutoka mataifa ya Hispania na Ujerumani.
No comments:
Post a Comment