Israel yaikashifu Argentina kuhairisha mechi
Lionel Messi, nahodha wa timu ya taifa ya Argentina na amekuwa akilengwa na vitisho kutoka kwa raia wa Palestina
Waziri wa ulinzi wa Israel Avigdor Lieberman ameikashifu timu ya taifa ya mpira wa mifuu ya Argentina baada ya timu hiyo kutangaza kuahirisha mchezo wake wa kirafiki dhidi ya Israel uliokuwa umepangwa kuchezwa mjini Jerusalem.
Waziri Lieberman amesema kitendo kilichofanywa na Argentina ni kitendo cha kukubali kushindwa na kukubali kupandikisha chuki ya ubaguzi.
“Ni aibu kwa timu ya taifa ya Argentina kushindwa kuvumilia na kuhimili shinikizo kutoka kwa watu wanaoichukua nchi ya Israel,” aliandika kwenye ukurasa wake wa kijamii wa Twitter ikiwa ni kauli ya kwanza kutoka kwa Serikali ya Israel.
Awali ubalozi wa Israel nchini Argentina ulitangaza kuahirisha mchezo wa kirafiki uliokuwa umepangwa kuchezwa Jumamosi ya wiki hii, kwa kile Argentina imesema ni vitisho dhidi ya mchezaji wao Lionel Messi.
Mchezo huu wa kirafiki kuelekea fainali za kombe la dunia ulikuwa umepingwa vikali na raia wa Palestina ambao wanaamini kuwa eneo la mashariki mwa mji huo lilichukuliwa kwa nguvu na Israel na ndio makao makuu ya nchi yao.
Nchi ya Israel yenyewe inasema mji wote wa Jerusalem ni sehemu ya nchi yake na ndio makao makuu.
Uamuzi wa Argentina kuahirisha mchezo huo umekuja wakati huu jeshi la Israel likikosolewa vikali kwa matumizi makubwa ya nguvu dhidi ya raia wa Kipalestina kwenye eneo la mpaka wa Gaza ambako waandamanaji wamekuwa wakikabiliana na vikosi vya Israel.
Tangu mwezi Machi wananchi wa Gaza wamekuwa wakifanya maandamano kushinikiza kurejeshwa kwa eneo lao walilofukuzwa kwenye mwaka 1948 baada ya vita baina ya pande hizo mbili.
Waziri wa mambo ya nje wa Argentina Jorge Faurie akizungumza jijini Washington amesema anachofahamu ni kuwa hata wachezaji wa timu yao ya taifa hawakuwa tayari kusafiri kwenda Jerusalem kucheza mchezo huo kutokana na vitisho.
Kocha wa Argentina Jorge Sampaoli juma lililopita alinukuliwa akidai kuwa haoni sababu ya kusafiri kwenda Jerusalem wakati mchezo huo ungeweza kuchezwa jijini Barcelona ambako timu yake imeweka kambi kuelekea fainali za kombe la dunia.
No comments:
Post a Comment