Cristiano Ronaldo awaaga washikaji zake Madrid...
Kuna mengi nyuma ya pazia. Sasa imefichuka staa wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo aliwaambia wachezaji wenzake kabla ya mechi ya Liverpool ataondoka Real Madrid katika dirisha hili la uhamisho barani Ulaya.
Ronaldo aliingia katika shutuma kubwa kutoka kwa wachezaji wenzake wakiongozwa na nahodha, Sergio Ramos baada ya kuzungumza na waandishi wa habari mara baada ya mechi ya Liverpool na kudai ataondoka Real Madrid.
Inadaiwa wachezaji wa Madrid walichukizwa na Ronaldo alivyotumia vibaya sherehe yao ya ubingwa kutangaza kuondoka lakini tayari baadhi ya mastaa ambao ni marafiki zake wa karibu aliwaambia ataondoka mwishoni mwa msimu ulioisha.
Inadaiwa Ronaldo amechukizwa na kitendo cha kutopewa mkataba mpya na mabosi wa Real Madrid wakiongozwa na Rais Florentino Perez na staa huyo ameendelea kuwa chini ya hasimu wake, Lionel Messi na staa wa PSG, Neymar katika suala la mshahara.
Tangu Desemba mwaka jana, staa huyo ameinunia Real Madrid na klabu hiyo inaamini kwa sasa Ronaldo hastahili mshahara huo kwa sababu umri wake umekwenda na muda wowote kuanzia sasa makali yake yatashuka.
Ronaldo amedaiwa kutaka kurudi nyumbani Manchester United ambayo ilimuuza kwenda Real Madrid kwa dau la Pauni 80 milioni katika dirisha la majira ya joto mwaka 2009 huku akiweka rekodi mpya ya uhamisho ya dunia.
Hata hivyo, kumekuwa na utata mwingi kama kocha wa sasa wa United, Jose Mourinho atakuwa tayari kufanya kazi na Ronaldo ambaye hakuwa na uhusiano naye mzuri wakati walipofanya kazi kwa pamoja Santiago Bernabeu.
Kocha wa zamani wa Madrid na Timu ya Taifa ya England, Fabio Capello juzi alidai Ronaldo amedhamiria kuondoka Bernabeu katika dirisha hili la majira ya joto na amewekeza nguvu zake kurudi Old Trafford ambako amekuwa akiheshimika mpaka sasa.
PSG pia imedaiwa kuanza kumnyatia Ronaldo ambaye anaweza kujikuta akipishana na staa wa kimataifa wa Brazil, Neymar ambaye mabosi wa Madrid wanamuona kama mchezaji mwafaka wa kuwa nyota mpya wa klabu hiyo.
Inadaiwa Madrid ipo tayari kulipa kiasi cha Pauni 250 milioni kwa staa huyo wa zamani wa Barcelona na hivyo kuhitimisha zama za Ronaldo ambaye hakung’ara katika pambano la fainali dhidi ya Liverpool na badala yake ustaa wake ulichukuliwa na nyota wa Wales, Gareth Bale aliyefunga mabao mawili.
Kwa sasa Madrid haina kocha baada ya Zinedine Zidane kutangaza kuondoka klabuni hapo ghafla Ijumaa iliyopita lakini hata hivyo, hatima ya Ronaldo haitazamiwi kuamuliwa na kocha ajaye wa mabingwa hao wa mara tatu mfululizo Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.
Kwa sasa Ronaldo anatazamiwa kuungana na wenzake katika kambi ya Timu ya Taifa ya Ureno baada ya kupewa siku kadhaa za mapumziko baada ya pambano la fainali dhidi ya Liverpool, lakini ni wazi hatima yake itaamuliwa mara baada ya michuano ya Kombe la Dunia kumalizika kule Rusia Julai mwaka huu.
Ronaldo (33) kwa sasa anaweza kuwindwa pia na klabu za Marekani na China kutokana na jina lake kuwa kubwa kibiashara, lakini haionekani kama yupo tayari kupokea changamoto za kucheza soka la kulipwa nje ya Ulaya kwa sasa.
No comments:
Post a Comment