Aishi Manula gumzo kila Kona Kenya.
Nakuru. Kama kuna usajili ambao Simba itajivunia ni wa wachezaji wanne mastaa iliyowanyakua kutoka Azam mwaka jana.
Mastaa hao ni nahodha, John Bocco, mabeki Shomari Kapombe, Erasto Nyoni na kipa Aishi Manula.
Nyota hao wanne wamekuwa chaguo la kwanza kwenye kikosi cha Simba, lakini gumzo kubwa ni uwezo wa juu wa Manula katika kucheza mikwaju ya penalti.
Manula aliibeba Simba kwenye robo fainali ya mashindano ya SportPesa Super Cup juzi Jumatatu dhidi ya Kariobangi Sharks inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya.
Kipa huyo alidaka penalti mbili huku wapinzani wao wakigongesha mwamba moja, hivyo kuiwezesha Simba kusonga mbele kwa mabao 3-2.
Kila kona mjini hapa mashabiki wamekuwa wakizungumzia kiwango bora cha Manula katika kushika mipira hiyo inayopigwa kutoka umbali wa mita sita tu, lakini rekodi zinaonyesha kipa huyo ni hatari kwenye penalti.
Manula baada ya kujiunga na Simba Julai mwaka jana, wiki chache baadaye alionyesha kiwango bora kwenye penalti na kuipatia timu yake ubingwa wa Ngao ya Hisani mbele ya watani wao wa jadi Yanga.
Katika pambano hilo lililopigwa Agosti 23 mwaka jana, Manula alipangua penalti ya beki wa Yanga, Kelvin Yondani huku Juma Mahadhi akikosa.
Mbali na michuano hiyo, Manula aliibeba Azam kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) mwaka 2015 kwa kucheza penalti muhimu.
No comments:
Post a Comment