Trending News>>

MOKGWEETSI MASISI AAPISHWA KUWA RAIS MPYA WA BOTSWANA

GABORONE. Nchini Botswana aliyekuwa makamu wa Rais  Mokgweetsi Masisi ameapishwa kuwa Rais mpya katika taifa hilo teule lililopo kusini mwa bara Afrika, kufuatia aliyekuwa Rais wa nchi hiyo kumaliza muda wake.
Mapema leo April 01, 2018, Masisi alikula kiapo  mbele ya jaji mkuu, spika wa bunge la Botswana na mtangulizi wake Rais mstaafu Seretse Ian Khama.
Jaji mkuu wa nchi hiyo Maruping Dibotelo, ndiye aliyemuapisha Rais Masisi ndani ya Ikulu ya taifa hilo iliyopo  mji mkuu Gaborone, kisha akatoa hotuba kwa wananchi baada ya gwaride kuu la jeshi la ulinzi la Botswana kumaliza kutumbuiza.
Masisi mwenye umri wa miaka 55, anakuwa rais wa tano wa nchi hiyo. Anachukua nafasi ya kuliongoza taifa hili kubwa linalochukuliwa duniani kote kama alama inayoidhinisha demokrasia barani Afrika.
Aidha, Bunge la taifa la nchi hiyo litachagua Rais mpya katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka 2019.
Katiba ya Botswana inaruhusu utawala Rais kwa mihula miwili ya miaka mitano mitano, na inaruhusu makamu wa rais kuwa Rais kazi moja kwa moja iwapo Rais aliyekuwepo kamaliza muda wake.
Hata Rais aliyemaliza muda wake Ian Khama alichukua madaraka kutoka kwa aliyekuwa rais wa awamu ya tatu wa nchi hiyo Festus Mogae mwaka 2008 kabla ya uchaguzi uliokuwa ufanyike mwaka 2009 kwa utaratibu huo huo.
Rais Khama alimaliza muda wake hapo jana machi 31, 2018. Na amejijengea sifa kubwa duniani, alijulikana kama msemaji asiyegopa taifa lolote hasa kwa mataifa yaliyoendelea na amewahi kuwashutumu viongozi wa mataifa makubwa akiwemo Rais wa Marekani Donald Trump kwa madai amekuwa akidharau viongozi wa nchi za kiafrika.
Katika sherehe hizo Rais mpya Masisi alihutubia taifa na kugusia changamoto zilizopo na matarajio yake ambayo yeye kama kiongozi wa nchi anaenda kukabiliana nayo.
“Kama tunavyojua, Botswana inakabiliwa na changamoto nyingi kama vile ukosefu wa ajira, umaskini, uhalifu, VVU na UKIMWI,  matumizi mabaya ya pombe na madawa ya kulevya.
“Kwa hiyo, mojawapo ya vipaumbele vyangu vya juu kama Rais wa nchi hii nitashughulikia tatizo la ukosefu wa ajira hasa kundi la vijana ambao ndio wenye idadi kubwa ya wakazi wetu. Vijana tu katika nchi ni 60% ya wakazi wote nchi, hawa ni viongozi wa baadaye na kwa hiyo kuwekeza katika hawa ni kujenga daraja ya baadaye.” Alisema Rais Masisi.
Masisi ni mwanachama wa chama cha Botswana Democratic Party (BDP), kitaaluma ni mwalimu, ana digrii moja aliyoipata huko Florida state University. Awali alikuwa akifanya kazi ya kufundisha katika Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa kwa miaka minane hadi 2003 kabla ya kuingia katika siasa, baadae alichaguliwa kuwa mbunge mwaka 2009.
Katika utumishi; Rais Masisi, alihudumu katika ofisi ya rais kama waziri wa masuala ya umma tangu mwaka 2011 hadi 2014,baadae aliteuliwa kuwa waziri wa elimu nafasi aliyoishika mpaka baada alikuwa makamu wa Rais mwaka jana 2017.
Botswana ni nchi yenye utajiri mkubwa wa almasi pia ni moja mataifa yenye usimamizi mzuri wa kiuchumi unatokana na kujitegemea zaidi katika maliasili za ndani.
Botswana ilijipatia uhuru wake mwaka 1966, imekuwa na mfumo wa uongozi wa kidemokrasia kwa miaka mingi, ikiwa na viongozi ambao huchaguliwa kwa kura ya wananchi. Watu wa Botswana hujiita ‘Batswana’, hii ni kutokana na jina la kabila kubwa nchini humo ambalo ni karibia asilimia 79 ya wakazi wote.

No comments:

Powered by Blogger.