Trending News>>

Moyo wa Dhahabu- Sehemu ya 01( Simulizi ya Kweli)

Written By Bigie 

Mwandishi:Grace Godfrey Rweyemam
Siku kadhaa zilizopita, nilimtembelea rafiki yangu mmoja Consoler. Huenda wengi mmemsikia, au mnamfahamu. Huyu ni mwanamke mdogo anayelea wasichana wanaoishi mazingira magumu, na anaishi nyumbani kwake na mabinti zaidi ya thelathini. Siku hiyo kwa bahati nilikutana na dada mmoja nyumbani kwake, ni mjamzito, aliyekaa kwenye ndoa yake kwa miaka nane kabla ya kubeba hiyo mimba aliyonayo. 


Katika mazungumzo, alinifahamu mimi kama mwandishi, na akatamani sana ningeandika simulizi ya kumuhusu katika hizi simulizi ninazoandika. Kujua kuwa ilimchukua miaka nane kabla ya kubeba ujauzito, ilinifanya nivutiwe kusikia hadithi ya maisha yake, lakini nikimsikiliza, niligundua kuwa lengo lake halikuwa kusema sana kumuhusu yeye mwenyewe. Tulipanga na kuonana, tukazungumza kwa kirefu sana, nami kweli nikaona vema kuweka simulizi hiyo ya maisha ya huyo binti Neema Mashauri kati ya hizi simulizi za kila wiki, kwani kwa kiasi kikubwa imenifundisha mambo mengi.

“Sio wote wenye mbio washindao, na wala si wote wenye juhudi wafanikiwao. Awali sikuelewa uhalisia wa hizi sentensi, na hata mtu angenishawishi vipi, nisingeamini ni ukweli. Niliamini sana katika jitihada zangu binafsi. Nikiwa shuleni, nilifanya vizuri, ila ni kwa sababu nilikuwa msikivu sana darasani na nilijisomea. Sikuwahi kufeli kwenye mitihani mikubwa, yaani ya taifa, na elimu yangu ilikuwa ya moja kwa moja pasipo kukwama popote. Niliamini pia kwa ufaulu wangu ningepata kazi kiurahisi tu, sasa hapo kukawa na tatizo kidogo. 

Nikaamua niendelee kusoma, nikamaliza shahada ya pili, na ya tatu, ila bado kupata kazi haikuwa rahisi. Nikaanza kufikiri, kumbe mtu unaweza usome na ufaulu vizuri halafu usipate kazi. Ila bado nilijipa moyo kuwa walau ni msomi. Jinsi ambavyo mtu aliyesoma hufikiri, siyo kama asiyesoma, niliwaza, na nilikuwa na hakika kwamba kuna siku nitapata kazi nzuri na kufikia maisha ninayotamani.

Wakati huo nilikuwa nimeolewa tayari, kwani niliolewa nikiwa ninasoma shahada yangu ya pili. Pia katika ndoa niliamini kuwa nikiolewa tu, kwa wakati wowote ninaohitaji ningepata mtoto. Tukakubaliana na mume wangu kuwa tuwe na mwaka mmoja wa fungate, halafu tuzae watoto wawili au watatu tu baada ya huo mwaka, nikiamini kuwa hapo ningekuwa tayari na kazi nzuri na kuwapa wanangu maisha ninayotaka. Miezi sita ya ndoa ilipopita, nilianza kuhisi kuwa nahitaji mtoto, na mume wangu vilevile, tukakubaliana tuanze kutafuta. Mwaka wa kwanza uliisha, na wa pili, nikasema labda kwa kuwa bado sina yale maisha ninayohitaji ndio sababu Mungu hajatupatia mtoto. 

Niliongeza bidiii kutafuta kazi huku nikiwa nasoma shahada yangu ya tatu (PhD), huku tukiendelea kutafuta mtoto. Miaka iliendelea mbele, nikamaliza masomo tukiwa bado hatuna mtoto. Nilianza sasa kujiona ni kama mtu mwenye mkosi, kwani kila ninachotamani hakifanikiwi.

Nilianza kuwa namlaumu Mungu kwa kuninyima kila ninachomuomba. Nilikuwa mwenye kisirani na kukasirishwa na jambo lolote dogo ambalo ningefanyiwa, hasa na mume wangu au watu wangu wa karibu, huku nikilaumu kwamba ni kwa sababu sina kazi na sina mtoto. Baadaye nilibahatika kupata vikazi vidogo, visivyoendana kabisa na elimu yangu, na vyenye pesa kidogo. 

Nilifanya tu sababu sikuwa na kazi, lakini kisirani kilinizidi, kwani sasa nilichoka sana na bado majukumu ya nyumbani yalinihitaji na sikuwa na pesa ya kutosha. Tuligombana mara kwa mara na mume wangu kwa ajili ya kisirani changu, ndoa nayo ikaanza kunichosha. Nilikuwa mkristo, ninayeenda kanisani vizuri, ila mara zote nilisema ukristo wangu hauna faida kwani haukunizalia matunda.

Kuna siku ilitokea nilitakiwa kufuata kitu fulani mjini, na gari yangu ndogo. Nikawasha redio kwenye gari, nakumbuka ilikuwa siku ya wanawake duniani na redio ya CloudsFM Radio nadhani walikuwa wametafuta mwanamke wa nguvu kwa kuangalia wanawake wanaofanya mambo makubwa nchini. 

Aliyeshinda ni huyu dada Consoler Eliya Wilbert. Sikuwa nimeanza kusikiliza hicho kipindi mapema hivyo nilikuta wanamalizia, lakini kwa kiasi nilichosikiliza, niligundua walimzungumzia Consoler kama mwanamke wa ajabu sana. Mwanamke huyu alitajwa kama mdogo kwa umri, na alikuwa akiishi na mambinti walioishi kwenye mazingira magumu zaidi ya thelathini nyumbani kwake, tena kwenye nyumba ya kupanga, na aliwahudumia bila kuwa na mdhamini yeyote wa kudumu mbali na wananchi walioguswa tu na kumpelekea msaada.

Nakumbuka kabla sijashuka kwenda nilipokuwa naenda, nilikaa kwenye gari dakika kadhaa nikitafakari sana juu ya huyo mwanamke wa nguvu, nikajikuta natoa machozi. Ingawa sikuwa nimemfahamu kiundani, au kujua kile anachofanya, lakini ile kufikiri tu kuwa kuna mwanamke anaishi na idadi ya watoto wote hao nyumbani kwake, bila uhakika wa kupata pesa ya kuwalisha na kuwatunza, nilishangaa ni moyo wa namna gani. 

Nilianza kujilinganisha nikajikuta nikijionea aibu mwenyewe, kwani licha ya kuwa nina kazi isiyonilipa vizuri, sikuwahi kuwaza juu ya nitakula nini au eti nimeishiwa pesa ya chakula. Ingawa kuna aina fulani ya maisha sikuridhika kabisa kuwa nayo, lakini maisha yangu yalikuwa bora sana kulinganisha na watu wengi wenye mahitaji. Mara nyingi nilijiahidi kuwa nitakapopata pesa na kazi ninayoitamani, nitakuwa nikihudumia yatima na wajane, na nilihisi kwa hali yangu ya uchumi nilikuwa sahihi kutotoa msaada kwa watu wenye uhitaji.

Niliamua kuwa ni lazima nimtafute Consoler, nione ni mtu wa namna gani, na hapo ndipo nilipokutana na mwanamke ambaye kwakweli sikuwahi kuhisi kama mtu wa namna hiyo anaweza akawepo duniani. 

Consoler yuko mbioni kutoa kitabu cha maisha yake, ambacho ninaamini kitakuwa na mambo mengi sana ya kufaa watu wajue. Ila nadhani sitajizuia kuzungumza kwa upana kumuhusu ninapozungumzia pale nilipo leo hii, kuanzia siku nimeonana naye. Katika simulizi langu, sehemu ya historia yake ambayo ningependa iandikwe imenisababishia badiliko kubwa mno, na kamwe sitaacha kumtaja huyu mwanamke mdogo kama mwanamke wangu wa nguvu.

Nilikutana na watoto wengi wa kike, walionipokea nikishuka kwenye gari, wakapokea mizigo yangu kidogo niliyokwenda nayo. Ilikuwa siku ya Jumapili, na tofauti na vituo vingi vya kulea watoto, mabinti hawa walivaa vizuri tu. Niliingia ndani, sebuleni, nikajisikia huruma kiasi, kwani kwa nyumba ya wanandoa vijana, ningetaraji kuona namna fulani ya muonekano. 

Kulikuwa na makochi machache, yaliyochakaa sana, na televisheni ukutani. Hiyo ndiyo sebule yake, na muonekano wa nyumba yake ukiwa wa hali ya kawaida kabisa. Hakukuwa na ufahari hata kidogo, palikuwa na taraza zilizochakaa sana chini. Nyumba haikuwa ndogo, lakini haikuwa nyumba ya kuwatosha watu thelathini na sita walioishi na kulala hapo kama familia moja.

Kitu kingine kikanishangaza sana, nilipomuona Consoler mwenyewe na kuona kwamba kiumri mimi nilikuwa mkubwa kumzidi. Ingawa nilijua ni mwanamke mdogo ila sikudhani kama angepungua miaka arobaini kwa namna nilivyomsikia. Picha yangu kichwani ilikuwa ya mwanamke wa miaka kama arobaini mbili mpaka na tano hivi, lakini kumbe alipata miaka thelathini na mitatu tu. 

Binti huyu aliyekuwa na miaka nane ya ndoa yake wakati huo, alikuwa ni kama mama mzoefu aliyezaa watoto wengi. Kila binti alionekana kuwa mwanae, siyo kwa kuigiza. Wadogo kwa wakubwa, walikuwa huru sana. Walionekana wenye furaha na kila mmoja nilimsoma kuwa alimpenda huyo mama yao, si kwa unafiki.

ITAENDELEA ...

No comments:

Powered by Blogger.