Trending News>>

Serikali yatoa agizo kwa Wananchi dhidi ya Hospitali



Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto imewataka wananchi kutoa taarifa kwa hospitali yeyote inayotoza fedha kwa ajili ya matibabu ya wajawazito wanaokwenda kupatiwa matibabu kwa kuwa huduma hizo zinatolewa bure.

Tamko hilo limetolewa na Naibu wa Waziri wa wizara hiyo Dkt. Faustine Ndugulile,  katika mkutano wa 10 kikao cha tano cha Bunge kinachoendelea mjini Dodoma wakati alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu Hawa Mchafu Chakoma alipotaka kujua serikali ili kuwa ina maana gani kusema matibabu kwa wamama wajawazito ni bure.

"Mama wajawazito ni moja ya makundi maalum wanaopaswa kupata huduma za matibabu bure kama ilivyoainishwa katika muongozo wa uchangiaji wa huduma za afya mwaka 1997. Wakina mama wajawazito ni haki yao kupewa huduma zote bila ya malipo na sio zile tu zinazohusu ujauzito", amesema Dkt. Ndugulile.

Pamoja na hayo, Dkt. Ndugulile ameendelea kwa kusema "katika muungozo uliopitiwa mwaka 2009-2010 imetamkwa bayana huduma ya afya kwa mama wajawazito ni bure ikiwa inamaana mara tu mwanamke anapokuwa mjamzito huduma zote kuanzia kliniki ya wajawazito, pale atakapougua maradhi yeyote pamoja na huduma ya kujifungua sanjari na kumuona daktari, kupatiwa vipimo, kupatiwa dawa, kufanyiwa upasuaji pale itakapo hitajika kufanyika hivyo".

Aidha, Dkt. Ndugulile amesema wizara ya afya imeandaa bajeti ya kununua vifaa wanavyotakiwa kutumia wanawake wajawazito ili kuwaondolea adha wafika hospitalini.

"Wizara imeandaa bajeti kutumika kwa ununuzi wa vifaa vinavyohitajika wakati wa kujifungua kwa maana 'delivery parts'. Vifaa hivyo watapewa wakina mama wajawazito wanapokaribia kujifungua ili wawe wanatembea na vifaa hivyo na kupunguza kero kwa kina mama kujinunulia vifaa vyao wao wenyewe", amesisitiza Dkt. Ndugulile.

Kwa upande mwingine, Dkt. Ndugulile amesema serikali inazikumbusha halmashauri kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sera hiyo ili wakina mama wajawazito wapate huduma ya kujifungua bure kama muongozo wa uchangiaji wa mwaka 1997 na sera ya afya  ya mwaka 2007 inavyoelekeza.

No comments:

Powered by Blogger.