Waziri Lukuvi amaliza mgogoro wa ardhi Vingunguti
Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi
ameumaliza mgogoro wa ardhi wa muda mrefu kati ya wakazi wa Mtaa wa
Mtambani Vingunguti na mwekezaji wa kampuni ya PMM jijini Dar es salaam.
Mwekezaji
huyo wa Kampuni ya PMM inayojihusisha na uhifadhi wa mizigo alitaka
kuchukua eneo la hekari 228 lenye nyumba 4,000 na wakazi 70,000 wa Mtaa
wa Mtambani Vingunguti.
Waziri
Lukuvi amesema Serikali haitambui uwekezaji uliokuwa ufanyike na
kwamba, mwekezaji hakufuata utaratibu uliyowekwa na Serikali, hivyo
kusababisha mgogoro huo kuwa mkubwa.
Kwa
mujibu wa wananchi wa eneo hilo tangu mwaka 2012 mwekezaji huyo
aliwazuia kufanya shughuli zozote za uendelezaji kwa kile alichodai
ameshafanya tathmini na anaisubiri Wizara ya Ardhi ambayo
inamchelewesha, jambo ambalo Waziri Lukuvi amekanusha.
Mwekezaji
huyo ametakiwa kurejesha nyaraka alizozichukua kwa wananchi hao kinyume
na utaratibu na ametakiwa kuwalipa fidia wananchi kwakuwa aliwazuia
wakazi hao kufanya shughuli zozote za uendelezaji kwa kile alichodai
ameshafanya tathmini. Hata hivyo, hadi sasa hakuna kinachoendelea na
malipo hayajafanyika.
Waziri
lukuvi aliwaambia wananchi hao kuwa kuanzia leo haya maeneo ni mali ya
wananchi kama anataka kununua aanze upya kufuata utaratibu uliowekwa, na
haiwezekani mtu anakuja kuwanunua watu 70,000 kienyeji.
“Hatuzuii
mtu kuuza mali yake, tunachosimamia sisi ni haki itendeke na utaratibu
ufuatwe, lakini katika mchakato huu mambo yamekwenda ndivyo sivyo,” amesema Waziri Lukuvi.
Kwa
upande wa meneja wa mradi wa PPM Bwana Deogratius Chacha amesema wapo
katika hatua za mwisho na malipo yangefanyika ndani ya siku 90 zijazo
ambapo wananchi hao hawakukubaliana na hilo.
Wakazi
wa eneo hilo wamemwambia waziri Lukuvi kuwa mwekezaji amechukua pia
leseni zao za makazi kwa muda mrefu na kushindwa kuendeleza makazi yao.
Hata hivyo, hadi sasa hakuna kinachoendelea na malipo hayajafanyika
zaidi ya ahadi na kwamba anasema Wizara ya Ardhi ndio inayomchelewesha.
Kauli
hiyo imemfanya waziri Lukuvi kutoa agizo kwa meneja huyo kuwarudishia
nyaraka zao wakazi wote hadi ifikapo kesho saa tano asubuhi. “OCD
chukua vielelezo vya meneja, hakikisha hadi kufikia kesho saa tano awe
amewarudishia wananchi nyaraka zao, kinyume cha hapo mkamate mweke
ndani,” amesema waziri Lukuvi.
Na Hassan Mabuye, Wizara ya Ardhi
No comments:
Post a Comment