Wanajeshi waliomng'oa Mugabe madarakani wateuliwa Baraza la Mawaziri Zimbabwe
Rais
mpya wa Jamhuri ya Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa ametangaza baraza la
mawaziri ambapo amewateua viongozi wakuu wa jeshi la nchi hiyo katika
nafasi mbalimbali.
Katika
baraza hilo lililotangazwa Novemba 30, Mnangagwa amemteua Meja Jenerali
Sibusiso Moyo kuwa Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi. Moyo ndiye
alitangaza katika kituo cha runinga cha Taifa (ZBC) kuwa jeshi
limechukua udhibiti wa nchi wakati Rais Mugabe alipowekwa kizuizini
nyumbani kwake.
Aidha,
Mkuu wa Jeshi la Anga la Zimbabwe, Perence Shiri ameteuliwa katika
baraza hilo na kuwa Waziri wa Kilimo na Masuala ya Ardhi.
Mnangagwa aliapishwa juma lililopita kuwa Rais wa Zimbabwe baada ya Robert Mugabe kukubali kujiuzulu.
Wakati
akihutubia mjini Harare baada ya kuapishwa, Mnangagwa aliahidi
mabadiliko makubwa, lakini baraza lake la mawaziri limekosolewa vikali
kutokana na uwepo wa viongozi hao wa jeshi.
Jeshi
la Zimbabwe limekuwa na mchango mkubwa katika aina ya siasa za nchi
hiyo, na mara kadhaa limekuwa likikosolewa kwamba, lilimsaidia Rais
Mugabe kukaa madarakani kwa miaka 37.
Mbali
na uteuzi wa wanajeshi hao, lakini pia baraza hilo limekosolewa kwa
kuwapo kwa baadhi ya watu ambao walikuwa na uhusiano na Rais Mugabe,
mfano Chris Mutsvangwa ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari.
Wengi
waliotoa maoni yao wamesema kuwa hatua hiyo imewakatisha tamaa kwa
waliamini uwepo wa kiongozi mpya ungeifanya nchi hiyo kupata viongozi
wapya ambao wangesaidia kuitoa Zimbabwe hapo ilipo sasa.
No comments:
Post a Comment