TIMU YA AZAM KUMPELEKA MBARAKA YUSUPH AFRIKA KUSINI KWA MATIBABU
MSHAMBULIAJI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC,
Mbaraka Yusuph, anatarajia kuondoka nchini kesho Jumatano jioni kuelekea
jijini Cape Town, Afrika Kusini kwa uchunguzi wa goti lake la kushoto
baada ya kuumiza ‘meniscus’ (washa).
Yusuph
alipata majeraha hayo akiwa na timu ya Taifa ya Tanzania Bara
‘Kilimanjaro Stars’ wakati ikicheza na Libya kwenye mchezo wa michuano
ya Kombe la Chalenji ulifanyika nchini Kenya Desemba 3 mwaka huu.
Akizungumza
mbele ya waandishi wa habari leo, Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd,
alisema kuwa tayari uongozi wa timu hiyo wameridhia na atakwenda
sambamba na Makamu Mwenyekiti, Abdulkarim Nurdin ‘Popat’, atakayekuwa
akishughulikia taratibu zake zote za matibabu.
“Mbaraka atakwenda kufanyiwa kwanza uchunguzi zaidi baada ya
kupata uchunguzi wake na kupata majibu kwamba ni kitu gani kinamsumbua
zaidi wao ndio watajua kuwa Mbaraka anahitaji operesheni au atapewa tiba
mbadala,” alisema.
Katika
hatua nyingine, Jaffar alithibitisha kuwa tayari timu hiyo imepokea
vibali vya kufanya kazi nchini kwa mshambuliaji mpya wa timu hiyo,
Bernard Arthur, ambaye sasa ni rasmi ataruhusiwa kucheza kwenye mchezo
ujao wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Area C
United ya Dodoma utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumamosi hii saa
1.00 usiku.
“Bernard
Arthur yupo huru kucheza mashindano yote ambayo yanahusu Azam FC kwa
maana kwamba taratibu za kupata vibali vyake vya kufanya kazi nchini
zimekamilika, sisi Azam FC tunamatumaini kwamba kwa kushirikiana na
wenzake atatoa mchango mkubwa na vilevile kuweza kuhakikisha kuwa safu
yetu ya ushambuliaji itazidi kuchangamka zaidi,” alisema.
Arthur
amesajiliwa akitokea Liberty Professional ya Ghana kwa mkataba wa miaka
miwili, ambapo hadi sasa ameshafunga mabao matatu kwenye mechi za
kirafiki alizocheza akifunga la kwanza dhidi ya Friends Rangers katika
sare ya bao 1-1 kabla ya kutupia mawili, Azam FC ilivyoilaza Villa Squad
mabao 7-1.
No comments:
Post a Comment