Shibuda amuomba Rais JPM kuvipiga jeki vyama visivyopata ruzuku
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa
nchini ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Ada Tadea, John Shibuda,
amemuomba Rais John Magufuli kutoa fedha za ruzuku kwa vyama vya siasa
visivyopata ruzuku, ili viweze kushiriki katika uchaguzi wa marudio
kwenye majimbo matatu unaotarajiwa kufanyika Januari 13,2018.
Shibuda ametoa ombi hilo leo Disemba 18
kwenye Mkutano Mkuu wa tisa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambapo amesema
hadi sasa kuna vyama vya siasa takribani kumi vilivyotangaza kushiriki
uchaguzi huo, huku akimuomba Rais Magufuli kukipa kiasi cha milioni 60
chama chake cha Ada Tadea ili kiweze kushiriki uchaguzi wa marudio.
Katika hatua nyingine, Shibuda
amevishangaa vyama vya siasa vya upinzani vilivyosusia kushiriki
uchaguzi wa marudio pamoja na kutohudhuria kwenye sherehe za kitaifa
licha ya kupewa fedha za ruzuku na kuwaita kuwa si wazalendo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UDP, John
Cheyo amevipasha vyama vya siasa vilivyotangaza kususia uchaguzi kuwa,
uamuzi huo hautawezi kuiondoa CCM madarakani.
“Wanaoshindana na CCM wajue kwamba
CCM linatisha tusitumie muda mwingi kuliangusha, na ukitaka kuliangusha
ujue uko wapi lisije likakuangusha. Wisi ni watanzania na mama yetu ni
Tanzania, mwanasiasa anayeishambulia Tanzania si mzalendo. Tunaoshindana
nawaomba tuangalie Tanzania kwanza tuache mchezo wa kususia susia,
hatuwezi kuiondoa CCM kwa mchezo huo,” amesema.
No comments:
Post a Comment