Naibu Waziri wa Kilimo aitaka NARI kuwaongezea malipo wafanyakazi
Kaimu
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele (NARI) ambayo
Kitaifa inaratibu Utafiti wa zao la Korosho, Mbegu za mafuta na mazao
jamii ya mizizi (Muhogo na viazi vitamu) Dkt Omari Mponda ameagizwa
kuwaongeza malipo ya kazi wafanyakazi wa kituo hicho katika mradi wa
kubangua Korosho.
Agizo hilo
limetolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa leo 22
Disemba 2017 wakati akizungumza na wafanyakazi wa kituo hicho cha
Utafiti Mara baada ya kutembelea kiwanda kidogo cha kubangua Korosho na
kubaini kuwa wafanyakazi hao wanalipwa shilingi 600 kwa kila kilo moja
ya korosho wanayobangua kiasi ambacho hakiakisi ufanisi wa kazi kubwa
wanayoifanya.
Katika
maelekezo yake Naibu Waziri huyo amemuagiza Kaimu Mkurugenzi wa kituo
hicho kuongeza kiasi cha malipo walau kufikia shilingi 1000 kwa kila
kilo moja wanayobangua ili wafanyakazi hao waweze kupata malipo ambayo
yatamudu gharama za maisha.
Sambamba na
hayo pia ameupongeza Uongozi wa kiwanda hicho kwa kubuni ajira hizo mpya
za mradi huo wa korosho zinazowanufaisha wananchi wa Mtwara sambamba na
pongezi za kuajiri wafanyakazi wengi ambao asilimia kubwa ni wanawake.
Aidha,
amesisitiza kuongeza bidii ya utoaji Elimu kwa wananchi kufahamu umuhimu
wa mazao ya muhogo, Njugu na Mbaazi ili yaweze kutumika zaidi kwani ni
fahari kwa wakulima na wananchi kwa ujumla.
Katika hatua
nyingine Mhe Mwanjelwa ameipongeza Taasisi hiyo kwa kufanya Tanzania
kuwa nchi ya kwanza Afrika kutoa/kugundua na kusajili mbegu bora 54 za
korosho kwa ajili ya matumizi kwa wakulima mwaka 2006 (Aina 16), Mwaka
2015 (Aina 22 mbegu chotara), na Mwaka 2016 (Aina 16 mbegu fupi).
Alisema Aina
hizo za mbegu hizo zina uwezo wa kuzaa korosho nyingi na bora, Zina
uwezo wa kuvumilia magonjwa na wadudu waharibifu na kufanya Utafiti
kupendekeza zaidi ya Aina 30 za viuatilifu vya kudhibiti visumbufu vya
Korosho.
Taasisi ya
Utafiti wa kilimo Naliendele (NARI) imepewa jukumu la kufanya Utafiti
ili kuongeza tija katika Kilimo katika kanda ya kusini mikoa ya Lindi,
Mtwara na Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma.
Na Mathias Canal, Mtwara
No comments:
Post a Comment