Maji, Vyoo nichangamoto katika Vituo vya Afya Vijijini
Hali ya upatikanaji wa majisafi na salama pamoja na vyoo katika vituo vya huduma za afya maeneo ya vijijini bado ni changamoto, huku asilimia 44 pekee ndio vina huduma hiyo.
Kati ya hizo, asilimia 34 ya vituo hivyo vimebainika kuwa bado vinatumia maji kutoka katika vyanzo ambavyo si salama, ambavyo ni mito, maziwa, visima visivyofunikwa na mabwawa, huku asilimia 56 zikikosa kabisa uwapo wa huduma hizo muhimu.
Takwimu hizo ni kwa mujibu wa utafiti wa tathmini ya upatikanaji wa huduma muhimu katika vituo vya afya wa mwaka 2014/15 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na wadau wengine.
Ili kukabiliana na hali hiyo, jana Serikali imezindua Mwongozo wa Taifa wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira katika vituo vya afya.
Mwongozo huo umezinduliwa na Mkurugenzi wa Uratibu wa Kisekta wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dk Andrew Komba kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubsya.
Akizungumza kuhusu mwongozo huo, Mratibu wa Kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira, Anyitike Mwakitalima alisema umeandaliwa kuboresha utoaji huduma katika vituo vya afya nchini.
“Sekta ya afya inakabiliwa na changamoto nyingi kwa muda mrefu kutokana na kutokuwapo kwa mwongozo wa Taifa ambao utasaidia kusimamia ubora wa utoaji huduma katika vituo vya afya ikiwamo ujenzi wa vyoo bora na upatikanaji wa maji safi.
“Tulibaini pia asilimia 42 ya vituo havina sehemu maalumu za kunawia kwa ajili ya watoa huduma za afya kunawa mikono katika vyumba vya kujifungulia, hali hii ni mbaya ikiwa hatutachukua hatua, kuna uwezekano wa watoto wanaozaliwa kupata athari mbalimbal,” alisema.
Awali, Dk Komba alisema mwongozo huo utasaidia Serikali na wadau wa maendeleo kusimamia na kutekeleza masuala ya usafi wa mazingira.
“Mwongozo unatoa maelekezo stahiki namna ambavyo vituo vya afya katika ngazi zote vinavyopaswa kufanya katika upangaji mipango na uandaaji wa bajeti zitakazotumika katika usimamizi wa usafi wa mazingira,” alisema.
Mkurugenzi wa Mipango wa Shirika la WaterAid, Abel Deganga alisema kutokana na kukosekana kwa mwongozo kwa muda mrefu unaopima hali ya upatikanaji maji katika vituo vya afya nchini, utendaji kazi wa Serikali na wadau ulikuwa ukisuasua.
No comments:
Post a Comment