Trending News>>

Libya, badala ya kuwa mkimbizi unageuka kuwa ‘mtumwa’


Maelfu ya watu kutoka nchi kadhaa za Kiafrika, wengi vijana, wanazipa mgongo nchi zao na kutafuta bahati zao Ulaya. Hali ngumu za maisha katika nchi zao, umskini na migogoro na vita imewasukuma kutafuta hata njia za hatari na zisizokuwa za kisheria kufika Ulaya. Kuna waliofaulu na kutambuliwa rasmi kuwa wakimbizi walipofika Ulaya, lakini kuna wengi waliozama katika Bahari ya Mediterenia. Kuna wengi ambao wamepata masaibu makubwa hata kabla ya kutia mguu Ulaya.

Nchi ya Libya baada ya kupinduliwa utawala wa Muammar Gaddafi mwaka 2011, imegeuka kuwa “mchafukoge”, haina serikali iliyo imara na makundi tafauti ya kijeshi yamekuwa yakikabana roho. Hali hiyo ya fujo imewarahisishia watu kutoka nchi kadhaa za Kifrika kukusanyika katika miji iliyo kwenye mwambao wa Libya katika Bahari ya Mediterenia wakitamani waivuke bahari hiyo ili wafike Ulaya. Sasa Libya imekuwa ni kituo kukubwa kinachotumiwa na walanguzi wa biashara ya wanadamu kuwakusanya wateja wao wanaowaahidi kwamba watawafikisha “Mtoni” (yaani Ulaya). Makundi ya kijeshi katika nchi hiyo hushirikiana na walanguzi hao kuwakabidhi wakimbizi wa kutoka nchi mbalimbali za Afrika chini ya Jangwa la Sahara katika masoko na watu hao kuuzwa kama “watumwa”.

Kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Mataifa ni kwamba hivi sasa wanaishi Libya hadi Waafrika milioni moja wakitokea nchi zilizo chini ya jangwa la Sahara, zile za Ukanda wa Sahel, Somalia, Eritrea na Sudan. Maelfu yao wamezuiliwa katika kambi, tena chini ya hali ya kutisha isiyokuwa ya kiutu. Libya ilisaidiwa na Umoja wa Ulaya kwa kupatiwa boti za doria kulinda mipaka yake ya bahari na pia kuziokoa boti zinazobeba wakimbizi na ambazo ziko katika hatari ya kuzama. Msaada huo umewezesha kupungua idadi ya watu wa kutoka nchi chini ya Jangwa la Sahara kuivuka bahari kutoka watu 11,500 Julai na kufikia 6,300 Septemba mwaka huu. Hiyo ina maana kwamba idadi ya watu wanaoshikiliwa kwa nguvu katika makambi ya Libya imeongezeka.

Malalamiko ya serikali za nchi za Afrika na pia mashirika ya kutetea hali za binadamu yalizidi pale televisheni ya Kimarekani, CNN, ilipotangaza na kuthibitisha hapo Novemba 14 kuweko Libya kambi za minada ambapo wakimbizi kutoka nchi za Kiafrika huuzwa kama watumwa. Jambo hilo, licha ya kwamba limeiaibisha Libya, lakini limetoa sura kwamba kuna serikali za nchi nyingine za Kiafrika zisizojali nini kinawasibu Waafrika wenzio huko Libya. Lakini, ilipojulikana kashfa hiyo, angalau serikali ya Rwanda ilitangaza kwamba itakuwa tayari kuwachukua Waafrika 30,000 wanaoshikiliwa katika kambi hizo.

Wizara ya mambo ya kigeni ya Rwanda ilisema mwezi uliopita: “ Kama ilivyo dunia iliyobaki, Rwanda nayo pia imeshtushwa na picha zilizochapishwa na zinazoonyesha maafa yaliyoko huko ambapo Waafrika- wakiwamo wanawake na watoto- waliokamatwa walipokua njiani kwenda kutafuta himaya ya ukimbizi Ulaya wanashikiliwa. Kutokana na falsafa ya kisiasa ya Rwanda na kutokana na historia yetu wenyewe, sisi hatuwezi kunyamaza kimya wakati watu wanafanyiwa uovu wa kinyama wa kuuzwa kwa mnada kama vile wao ni wanyama wa mifugo.” Tangazo hilo la serikali ya Kigali liliendelea kusema: “Huenda Rwanda haiwezi kusema kwamba kila mtu anakaribishwa, lakini mlango wetu uko wazi.”

Gazeti la New Times la huko Kigali liliripoti baadaye kwamba serikali ya Rwanda na Umoja wa Afrika (AU) zimekubaliana kwamba nchi hiyo itachukuwa wakimbizi 30,000 na waziri wa mambo ya kigeni wa nchi hiyo, Louise Mushukiwabo, aliandika katika mtandao wa Twitter kuhusu Waafrika wanaouzwa huko Libya: ” Rwanda ni nchi ndogo, lakini tutatafuta nafasi kwa ajili yenu.” Inasemakana Rwanda pia inafanya mazungumzo na Israel ili kuwachukua Wasudan na Waeritrea waliokwama huko Israel walipokuwa njiani kwenda Ulaya kutafuta ukimbizi. Moussa Faki Mahamat, mkuu wa Kamisheni ya AU, ameipongeza hatua ya Rwanda na akazitaka nchi wanachama wa AU, sekta ya kibinafsi na raia wa Kiafrika kuwaunga mkono ndugu zao wanaosononeka na kuteseka huko Libya.

Mwezi uliopita huko Abidjan, Ivory Coast, ulifanyika mkutano wa kilele wa kawaida baina ya Umoja wa Ulaya na Afrika ambao ulijishughulisha sana na siasa ya uhamiaji pamoja na kashfa hii ya kuuzwa na kununuliwa watumwa huko Libya. Pia, serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa iliahidiwa kusaidiwa ili iondokane na kambi hizo. Kutokana na malalamiko kutoka mashirika ya kiraia, siku chache zilizopita nchi zaidi za Kiafrika zimeondosha mabalozi wao kutoka Libya na zimeutaka Umoja wa Mataifa na Mahakama ya Kimataifa ya The Hague zilishughulikie suala hilo la unyama na uhalifu unaofanywa Libya.

Habari ya kuweko makambi ya utumwa nchini Libya si mpya, ila sasa malalamiko yaliotolewa ni makali zaidi, na mbinu zinazotumiwa na hao walanguzi wa biashara ya wanadamu ni za kikatili zaidi. Pia, licha ya nchi za Ulaya kulalamika juu ya kuweko kambi hizo, lakini nchi hizohizo zinafunga kabisa milango kwa wakimbizi. Nchi hizo za Ulaya zinataka hata wale wanaoomba ukimbizi ambao tayari wameshakanyaga ardhi ya Ulaya warejeshwe makwao. Shirika la Umoja wa Mataifa juu ya Uhamiaji (IOM), limetaja juu ya kuweko masoko ya watumwa huko Libya na limesema kwamba mustakbali wa watu hao haujulikani, si leo wala si kesho. Wengi wao wako karibu na maeneo ya Kusini kabisa ya Ulaya. IOM ilisema isitarajiwe kwamba hali ya mambo itabadilika.

Kwa mujibu wa mashahidi walioshuhudia minada hiyo ya kuuzwa binadamu huko Libya ni kwamba katika masoko hayo watu huuzwa na kununuliwa, halafu hupelekwa kufanya kazi ngumu. Watu wanaofanya biashara ya magendo ya binadamu humuuza kila mkimbizi kwa dola 200 hadi 500. Pia, hulazimihswa kuwapigia simu jamaa zao ili watume fedha zitakazowezesha wajikomboe. Pale familia zao wanaposikia sauti zao zikilia ndani ya simu, baadhi ya wakati fedha hutumwa. Hivyo ndivyo walanguzi wa biashara hii inayoshamiri wanavyotajirika. Wakimbizi ambao hawana bahati ya kutumiwa fedha za ukombozi na jamaa zao hunyimwa chakula hadi wanakufa. Kwa mujibu wa IOM hayo ni maelezo ya watu walioko sasa Niger na ambao wamerejea kutoka Libya.

Libya iliyosambaratika, ambapo haijulikani serikali gani inayoshika hatamu ni taabu kuinusuru. Nchini humo hakuna sheria, kila mtu anafanya anavyotaka ni shida kukomesha uuzaji na ununuzi wa binadamu, licha ya kuweko malalamiko mengi duniani.

Mara nyingi wanasiasa hujifanya “hamnazo”, hujitoa kimasomaso, bila ya kujali kama wanasiasa hao ni Waafrika au Wazungu, hulipuuza tatizo hasa ambalo liko machoni mwao. Viongozi wa Ulaya na Afrika wanatambua kuwapo Waafrika wanaokimbilia Ulaya ni kutokana na hali ngumu ya maisha katika nchi wanakotokea.

Karibu tutaingia mwaka 2018. Mambo hayaonyeshi yatabadilika, watu zaidi watarajiwe watajaribu kwa kila njia kuingia Ulaya kuliko miaka iliopita. Watajaribu kuivuka Bahari ya Mediterenia kwa kutumia boti za mbao zilizo mbovu na kongwe. Kwa wengi wao bahari hiyo itakuwa kaburi lao. Baada ya baridi ya sasa kupungua kidogo Ulaya, msimu wa kuangamia Waafrika wengi katika bahari hiyo utaanza. Inanihuzunisha.

Source: Mwananchi

No comments:

Powered by Blogger.