Trending News>>

CHADEMA Watoa Kauli Kuhusu Kujiuzulu kwa Mbunge wa Siha, Molel


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA ) tarehe 14 Disemba,2017 tumepokea taarifa kupitia mitandao ya kijamii kuwa Mbunge wa Siha Dr.Godwin Mollel amejiuzulu uanachama na kujiunga na CCM.
 
Dr.Godwin Mollel ameeleza sababu ya uamuzi wake huo ni kutaka kulinda rasilimali za Taifa.
Sababu hii aliyoitoa ni ya kushangaza kwani Bunge ndicho chombo chenye wajibu wa kusimamia na kulinda rasilimali za Taifa kwa niaba ya wananchi.
Ni jambo la kushangaza kwa kuwa kitendo chake cha kulikimbia Bunge kama chombo cha kusemea na kutetea rasilimali za Taifa na kuja uraiani inatoa taswira gani maana kalikimbia Bunge lenye wajibu huo kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi yetu.
Tunawashauri wale wote ambao wanajitoa waeleze sababu halisi na sio kuhadaa umma kwa sababu uchwara kama hizi, maana wapo wanaosema wanaacha kazi kwenda kuunga mkono dhana ya ‘hapa kazi tu’ na wengine wanasema wanaenda kuunga mkono juhudi za kuboresha maisha kwa kuacha kazi.
CHADEMA tuko imara sana na tutaendelea na ajenda zetu bila kuyumbishwa na wimbi hili la watu wachache ambao wameamua kuwasaliti wapiga kura wao kwa kutoa sababu zisizo za msingi ambazo hazina maslahi kwa Taifa bali kwa maslahi yao binafsi . Huu ni ubinafsi wa hali ya juu.
Tutaendelea kujenga Taifa letu na Chama chetu bila kujali njaa za baadhi yetu wala maslahi ya watu wachache. Ila kwa hakika ni kuwa wale wenye dhamira thabiti ndio wataweza kufika mwisho wa safari ya kuleta mabadiliko salama. Ni dhahiri wale waliotanguliza ubinafsi hatutaweza kufika nao mwisho wa safari hii.
Imetolewa  Alhamis 14 Novemba, 2017 na ;
John Mrema,
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje.

No comments:

Powered by Blogger.