Unatamani Ndoa? Utaikuta Na Utaichoka!
NAMSHUKURU Mungu kwa kunilinda na kunijalia afya njema na pumzi ambayo amenipa bure. Bila kukusahau wewe msomaji kwa kuendelea kuunga mkono safu hii ya XXLove kwa maoni na ushauri wako. Moja kwa moja leo najikita kwa vijana ambao wengi wao wamejikuta wakitamani kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi au ndoa ingawa bado wengine umri wao unakuwa haujafikia.
Wapo vijana wengine ambao wamekuwa wakiambiana na kushauriana na wakubwa wao kuhusu athari za kuingia kwenye uhusiano wakiwa na umri mdogo, lakini bado hawataki kusikia wala kuelewa yaani hawaambiliki. Kuna baadhi ya mabinti wakiwemo wanafunzi na wasio wanafunzi ambao nao wamekuwa na tamaa hiyohiyo. Ni kama wanakurupukia mapenzi, wanatamani kuingia kwenye uhusiano, wakati umri wao bado haujafika. Wanatamani kuwa na wapenzi, wakati yawezekana ni wanafunzi au umri wao bado unaonesha hawajajitambua.
Hii ni hatari sana kwani kuna athari nyingi na mbaya kwa mabinti na hata vijana ambao wanajiingiza kwenye uhusiano kwa umri ambao siyo stahiki. Jamani mapenzi au ndoa ambayo unatamani kuipata, utaikuta tu, utaiishi na mwisho unaweza hata kuichoka, sasa kiherehere cha nini kukimbilia mapenzi wakati umri hauruhusu, wakati bado unasoma? Huo ni ushamba, huko ni kujitafutia matatizo makubwa na kuwasumbua wazazi siku yatakapowakuta ya kuwakuta. Hivi unadhani ukitundikwa mimba wakati bado uko kwenu, wazazi wako unawajengea picha gani kwa majirani au mtaani? Ni kuwashushia heshima wazazi wako, waonekane hawakukulea katika maadili yafaayo, lakini kumbe wewe mwenyewe unajifanya umeshindikana. Ukipata ujauzito ukiwa shuleni, serikali au walimu hawatakuacha salama!
Lazima utakutana na misukosuko ya hatari ambayo mingine itakufanya ujilaumu kwa hatua hiyo, mingine itakufanya utamani hata kujitoa uhai. Binti au kijana unayetamani kujiingiza kwenye mapenzi, hii ni elimu tosha kwako, achana na mapenzi, pigania kutimiza ndoto zako kwanza ndipo mengine yafuate. Ukiingia kwenye mapenzi kwa umri wako ulivyo ni ngumu sana kuhimili ‘stress’ za mapenzi na pia ukaweza kufanikiwa kufikia malengo yako. Ukitaka kuona maisha magumu, basi kubali kujiingiza kwenye uhusiano wa kimapenzi na wakati huohuo unasoma au unaishi na wazazi wako. Naliona sononeko la wazazi wako pindi utakapojazwa mimba ukiwa bado msichana mdogo, tena mwanafunzi wanayekuhangaikia ili uwe na maisha bora ya baadaye utakapojitegemea.
Naiona presha unayomsababishia mama au baba yako kwa gharama kubwa alizotumia kukusomesha, halafu leo anapokea taarifa kuwa mtoto wake kipenzi umenasa mimba! Naliona gonjwa la ajabu kwa mlezi wako baada ya kuzipata taarifa zako kuwa umefariki dunia wakati ukijaribu kutoa mimba kwa kuhofia dhihaka na kejeli shuleni na mtaani! Naiona chuki unayotengeneza baina yako wewe binti na wazazi, ndugu, marafiki na majirani, hasa baada ya kupewa ujauzito ukiwa mdogo au kuolewa kwa kujifanya unampenda bwana’ko. Nayaona maisha yako yatakavyokwenda kombo kwa muda kwa sababu umeacha shule na sasa unalea nyumbani huku bwana aliyekuzalisha akiwa hana lolote.
Nakiona kinjemba chako kikihaha kutoroka kijijini kukimbilia kwa kaka yake kisha kukutelekeza ukiwa huna mbele wala nyuma. WANAFUNZI KUWENI MAKINI NA UZINZI, KAMA NI NDOA MBONA IPO TU! HATA UZEENI UTAOLEWA NA PENGINE UTAICHOKA! Mwisho, wazazi msichoke katika kuwaelimisha vijana wenu kuhusu kuingia katika ndoa. Wafundisheni athari za kujiingia kwenye mapenzi kabla ya umri stahiki. Kwa maoni na ushauri, ni-follow Insta:@ mimi_na_uhusiano au jiunge na M&U WhatsApp kwa namba ya hapo juu.
No comments:
Post a Comment