Msuva, Samatta, ‘wapigana vikumbo’ mtandaoni
BAADA ya kufanya vizuri katika timu yake ya Difaa El Jadida ya nchini Morocco pamoja na timu ya taifa Taifa Stars, winga mshambuliaji Simon Msuva amempiku mshambuliaji Mbwana Samatta kws kuwa na wafuasi wengi katika ukurasa wa video wa YouTube.
Mwezi Julai mwaka huu Msuva alijiunga na klabu hiyo ya Morocco akitokea Yanga huku Samatta akiwa tayari amekubalika ndani ya kikosi cha Genk ya Ubelgiji tangu alipojiunga nayo Januari mwaka jana.
Kwa ujumla wachezaji hao wamejizolea mashabiki lukuki wanaofuatilia matukio yao katika kurasa mbalimbali za mitandao ya kijamii hasa kufuatia kufanya vema wanapokuwa katika klabu zao pamoja na timu ya Taifa Stars.
Imebainika kwamba katika ukurasa wake wa video wa YouTube unaojulikana kama Msuva Simon, Msuva amepata zaidi ya wafuasi 3,000 huku Samatta akiwa na wafuasi zaidi ya 2,000.
Idadi hiyo ni ya watazamaji waliojitokeza kuwaunga mkono katika kurasa hizo ambapo kwa kufanya hivyo wanapata fursa ya kuona kila video mpya inayowekwa kwenye kurasa zao.
Kwa upande wa kurasa za instagram, Samatta ana zaidi ya wafuasi laki tano (500,000) na kumpiku Msuva ambaye kwenye ukurasa huo ana zaidi ya wafuasi laki mbili (200,000).
Kwa upande wa mtandao wa twitter, Samatta amemzidi kete Msuva kwani ana wafuasi zaidi ya elfu hamsini (50,000) huku Msuva akiwa na zaidi ya wafuasi elfu moja (1,000). Msuva alichelewa kufungua ukurasa wa twitter ukilinganisha na Samatta.
Wakati huohuo ukurasa huo wa Samatta umependwa na zaidi ya watazamaji 1,000 huku wa Msuva ukipendwa na zaidi ya watazamaji 200.
Anachokifanya Samatta YouTube licha ya kuweka matukio yake ya uwanjani hasa mabao anayofunga katika Ligi ya Ubelgiji, Samatta amekuwa akipendelea kuweka kazi nzuri za wachezaji wengine kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Ikumbukwe hivi karibuni aliwahi kuweka video ya mabao mawili ya Msuva ambayo aliwafunga Botswana katika mechi ya kirafiki ambayo Stars ilishinda 2-0.
Mbali la hilo Samatta alishawahi kuweka video ya Emmanuel Okwi wakati alipoipatia bao Uganda hivi karibuni kwenye mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Misri.
Pia Samatta huwa anaweka video za magoli mazuri ya wachezaji mahiri wa Ligi mbalimbali za Ulaya.
Faida za mitandao kwa Msuva, Samatta
Zipo faida mbalimbali za wachezaji hao katika matumizi ya mitandao ya kijamii hasa ikitokea wakaitumia kwa njia zilizo sahihi.
Faida ya kwanza ni kipato kupitia mitandao, kwa mfano YouTube humlipa muhusika pindi anapofikisha watazamaji milioni moja katika ukurasa wake.
Hiyo ina maana kwamba wachezaji hao wanapaswa kuendelea kujituma uwanjani ili kujizolea mashabiki wengi watakaokuwa na hamu ya kuperuzi kurasa zao na hatimaye kufanikiwa kutimiza idadi hiyo itakayowafanya wawe wanakinga kiasi cha pesa kila mwezi.
Faida nyingine ni kusaidia kuwajengea uwezekano wa kazi zao kuonekana sehemu kubwa zaidi duniani na hivyo kuwapa urahisi wa kucheza soka katika nchi yoyote bila kikwazo chochote.
Mawakala wengi wa mchezo wa soka pamoja na wasaka vipaji huwa wanatumia kurasa maalumu za mitandao ya kijamii kuangalia uwezo wa mchezaji husika kabla ya kuanza kumfuatilia na kumfanyia majaribio.
No comments:
Post a Comment