MDOGO WA STEVEN KANUMBA AIELEZA MAHAKAMA JINSI KANUMBA ALIVYOFARIKI
Kesi ya mauaji inayomkabili muigizaji wa
filamu bongo Elizabeth Michael (Lulu) imeendelea kusikilizwa jana
katika Mahakama Kuu jijini Dar es salaam, kwa upande wa mshataka kuanza
kutoa ushahidi wao.
Akitoa ushahidi ndugu wa marehemu Steven Kanumba, Seth Bosco, alisimulia
mahakama jinsi ilivyokuwa siku ya tukio, na kwamba aligundua kuwa kaka
yake hapumui baada ya kugombana na mpenzi wake Lulu.
"Siku ya tukio marehemu Kanumba aliniambia nisitoke nyumbani anataka
tutoke wote kuanzia saa sita usiku, akaja Lulu na Kanumba ndiye
aliyemfungulia mlango Lulu, alipofika ndani nikasikia akimuuliza Lulu
kwanini anaongea na boyfriend wake mbele yake? Katika malumbano yao
Kanumba alikuwa akimvuta Lulu arudi ndani na Lulu naye alikuwa anataka
kutoka nje, wakati wakiendelea kugombana mlango wa chumba changu
sikuufunga”, alisikika Seth akiisimulia Mahakama.
Seth aliendelea kusimulia kuwa …..”Baada ya ugomvi Lulu alikuja chumbani
kwangu akilia, akaniambia Kanumba kadondoka amejaribu kummwagia maji
haamki. Na ilikuwa mara ya kwanza kuona ugomvi kati yao, nilipoingia
chumbani nilimkuta Kanumba chini kaegemea ukuta nikamlaza chali
nikamtafuta daktari wake, Dk Kageiya, alipofika alimfanyia chek up
akanambia ameshafariki ila akashauri tumpeleke hospitali ya Muhimbili”..
Hata hivyo, alipoulizwa na moja wa wazee wa Baraza, Rajabu Mlawa baada
ya kutoa ushahidi wake, kama anajua aliyesabisha kifo cha msanii huyo,
shahidi huyo alisema hajui.
Mzee wa Baraza: Katika kumchunguza kwako marehemu baada ya tukio hilo, ulibaini kwamba marehemu alipata madhara gani?
Shahidi: Madhara niliyoyabaini ni kukosa pumzi
Mzee wa Baraza: Hayo madhara ya kukosa pumzi yalisababishwa na ugomvi ule?
Shahidi: Kwa hilo mimi siwezi kujua nini kilisabisha kukosa pumzi.
Mzee wa Baraza: Umesema kuwa ulipokwenda chumbani kwa marehemu ulimkuta
ameanguka akiwa ameegemea ukutani, unajua ni nani alisababisha tukio la
kuanguka?
Shahidi: Siwezi kujua ni nani aliyesababisha kwa sababu mimi sikuwemo mle ndani
Wakati akihojiwa na wakili wa mshtakiwa, Peter Kibatala, kama alikuwepo
wakati sampuli za mwili wa marehemu zikichukuliwa kwa ajili ya vipimo
vya maabara, kama ilivyoandikwa kwenye maelezo yake, alisema hakuwepo.
“Mimi sikuwepo wakati wa kuchukua sampuli za mwili wa marehemu.
Alikuwapo ndugu yangu mwingine, mimi nilikuwepo kwenye mostmortem
(taarifa ya kitabibu ya chanzo cha kifo) ya kawaida.”
Wakili Kibatala: Kwa hiyo aliyeandika hapa alikuwa akibuni?
Shahidi: Siwezi kusema kuwa alikuwa akibuni, labda kama ungemuuliza mwenyewe.
Wakili: Katika maelezo yako Polisi ambayo uliyaandika muda mfupi tu
wakati wa tukio, kuna mahali ulipoeleza polisi kwamba ulipokwenda
kumfuata Dk Paplas ulimwambia mshtakiwa abaki na marehemu?
Shahidi: Hakuna mahali ambapo kuna kipengele nilipomweleza polisi kuwa
nilimuacha Elizabeth Michael na marehemu (Baada ya kusoma maelezo yake)
Hata hivyo, alipoulizwa tena na Wakili wa Serikali, George kuhusu kuwepo
kwa tofauti ndogondogo katika maelezo yake aliyoyaandika polisi na yale
aliyoyatoa kwenye ushahidi wake mahakamani, shahidi huyo alieleza kuwa
yeye alikuwa akihojiwa tu na aliyekuwa akiandika ni askari.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Sam Rumanyika iliahirishwa na
itaendelea tena leo kwa mashahidi wengine wa upande wa mashtaka kutoa
ushahidi wao.
Awali Wakili George aliieleza mahakama kuwa alitegemea kuwa na mashahidi
wawili jana, akiwemo Dk Kageiya, lakini wakati wakifanya mazungumzo na
shahidi huyo, aliwaeleza kuwa hajisikii vizuri na kuomba atoe ushahidi
wake kesho.
Pia Wakili George aliileza mahakama kuwa wataomba kuongeza shahidi mwingine ili wafikie watano.
No comments:
Post a Comment