Wanafunzi 22 Milambo Wafikishwa Mahakamani
Wanafunzi
22 wa Shule ya Sekondari ya Milambo ya mkoani Tabora wamepandishwa
kizimbani wakikabiliwa na mashitaka 12 matano yakiwa ya kujeruhi na saba
ya kuharibu mali, ambapo mmoja amesomewa tuhuma zake akiwa amelazwa
hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tabora Kitete.
Upande
wa serikali ukiongozwa na wakili Iddy Mgeni ulidai mbele ya hakimu
mkazi mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Tabora, Emanuel Ngingwana kuwa
washitakiwa walitenda makosa hayo 12 Agosti 14 mwaka huu majira ya
usiku.
Wakili
Mgeni alidai katika mashitaka ya kwanza hadi ya tano kuwa siku hiyo,
watuhumiwa kwa pamoja waliwashambulia na kuwajeruhi wakazi watano wa
kata ya Chemchem kinyume na kifungu namba 241 sura ya 16 kama
ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.
Aliwataja
walioshambuliwa na kujeruhiwa kuwa ni Juma Farahani, Iman Elias, Salehe
Ally na Ahmed Haruna wakazi wa mtaa wa Uhuru na Hamza Jafary mkazi wa
mtaa wa Dawa.
Katika
mashitaka ya sita na saba, walidaiwa siku hiyo watuhumiwa kwa pamoja
waliharibu mali ya Shaban Farahani chini ya kifungu namba 326 (1) cha
sheria ya makosa ya jinai huku wakijua kwamba ni kosa.
Upande
wa mashitaka ulidai katika mashitaka ya nane kuwa watuhumiwa waliharibu
vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh 440,000 zikiwemo spika mbili,
dirisha moja na simu mbili mali ya Hemed Rajab.
Wanafunzi
wa sekondari ya Milambo wanatuhumiwa kuvamia nyumba ya kulala wageni
iitwayo Nyakitonto na kuharibu taa tano na bango vyote vikiwa na thamani
ya Sh 750,000 mali ya Asia Maulid wakati katika shitaka la 10 ilidaiwa
kuwa watuhumiwa hao waliharibu turubai mbili, milango miwili, sahani na
vikombe, dirisha mbili, juzuu boksi tatu zinazotumiwa na waumini wa dini
ya kiislam mali ya Ally Juma, yote ikiwa na thamani ya Sh 4,278,000.
Watuhumiwa
wote walikana na mahakama ilisema dhamana ipo wazi na walitakiwa
wadhamini wawili kwa kila mtuhumiwa mmoja ambao watasaini mkataba wa
ahadi ya Sh milioni mbili kila mmoja na shauri hilo limeahirishwa hadi
Agosti 31, 2017.
No comments:
Post a Comment