Vigogo Wengine watano wamefikishwa Mahakamani leo Dsm
August 10, 2017 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, TAKUKURU
imewafikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu vigogo watano wa
zamani wa Shirika la Umeme Tanzania, Tanesco wakidaiwa kuhujumu uchumi
kwa kuisabishia Serikali hasara ya Tsh. Milioni 275.
Waliofikishwa Mahakamani ni pamoja na aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa
Tanesco, Robert Shemhilu, Ofisa Ugavi, Harun Mattambo, Mkurugenzi wa
Fedha, Lusekelo Kasanga, Mwanasheria wao, Godson Makia pamoja na
msambazaji kutoka kampuni ya M/S Young Dong Electronic Co. Ltd Martin
Simba.
Wakili wa Serikali, Vitalis Peter aliwasomea washtakiwa hao mashtaka
mawili ya uhujumu uchumi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,Thomas Simba ambapo
alidai kuwa kati ya January na December 2011 katika Ofisi za Tanesco
Ubungo, washtakiwa wakiwa waajiriwa wa Shirika hilo, walitumia madaraka
yao vibaya kwa kufanikisha malipo kwa msambazaji Martin Simba bila ya
kufanya uhakiki.
Aidha, Wakili Vitalis amedai kati ya January na December 2011 katika
Ofisi za Tanesco Ubungo, washtakiwa hao wakiwa waajiriwa wa shirika hilo
pamoja na msambazaji huyo waliisababishia Serikali hasara ya Tsh.
Milioni 275.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo washtakiwa waliruhusiwa kuongea kwa
sababu Mkurugenzi wa Mashtaka DPP amewasilisha Cheti maalum
kimachoiruhusu Mahakama kuisikiliza kesi hiyo ambapo walikana na upande
wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi umekamilika.
Hakimu Simba aliwataka washtakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika
ambao kila mmoja alisaini bondi ya Tsh. Milioni 40 huku mmoja kati ya
wadhamini hao akitakiwa kuwasilisha hati ya Mali isiyohamishika ambapo
walitimiza masharti hayo.
Washtakiwa hao watasomewa maelezo ya awali (PH) August 24, 2017.
No comments:
Post a Comment