Wanaokatiwa Bima wanauawa na waliowakatia ili wajitajirishe
Ni visa ambavyo vimewashangaza wapelelezi ambao waligundua wakati wakichunguza kundi la walaghai waliovamia sekta hiyo ya bima.
Maafisa
wa Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Bima (IRA) wa kuchunguza ulaghai
pamoja na wapelelezi wa kibinafsi ambao wamekodishwa na wadhamini,
waligundua msururu wa visa ambapo watu wanawaandikisha jamaa zao katika
bima mbalimbali za maisha pasipo kuwafahamisha, na kisha kupanga njama
ya kuwaua ili kulipwa mamilioni ya pesa za fidia kutoka kwa kampuni za
bima hizo.
Katika
kisa kimoja kilichowaacha wapelelezi vinywa wazi, meneja mmoja wa
zamani wa bima alimuandikisha mpwa wake maskini katika bima mbili,
lakini inadaiwa kuwa alipanga mauaji ya kijana huyo na kisha mwili
kutupwa barabara ya Kangundo kabla kukimbia kudai fidia.
Wachunguzi
hao waliozungumza na Taifa Jumapili, walisema mwanamume huyo aliibua
tashwishi alipotoa shinikizo chungu nzima kutaka alipwe fidia hiyo
akisema alihitaji pesa za kusafiri kuelekea Australia.
Afisa
huyo wa zamani wa bima, alikuwa amemchukulia mpwa wake mwenye umri wa
miaka 27 bima ya Sh10 milioni na nyingine ya Sh1 milioni katika kampuni
mbili tofauti. Alikuwa ametoa mchango mmoja pekee kabla mauaji hayo
kutokea.
Mwanamume
huyo alikuwa amefanikiwa kukamilisha utaratibu wa kupewa fidia ya bima
ya kwanza yenye kitita kinono, na alikuwa katika jitihada za kusaka
idhini ya kulipwa fidia ya bima ya pili tashwishi zilipoibuka.
Kumuua mpwa
Ripoti ya wapelelezi ambayo Swahilihub iliona,
ilimhusisha mshukiwa huyo katika mauaji ya mpwa wake, ambaye rekodi za
simu zilionyesha kuwa wawili hao walikuwa pamoja muda mfupi kabla kijana
kutoweka licha ya mshukiwa kukana hayo katika taarifa za kiapo.
Ripoti
ya upasuaji maiti iliashiria kijana huyo alifariki kutokana na jeraha
mbaya la kichwa lililosababishwa na maumivu yaliyoletwa na kifaa butu.
“Kutokana
na uchunguzi, ni bayana kuna ushahidi wa kuashiria kuwepo kwa Mauaji ya
Kujitajirisha yanayoendelezwa na wafadhiliwa,” wachunguzi hao
walihitimisha katika ripoti yao ya Juni.
Jamaa
huyo mshukiwa anasemekana kunaswa na vyeti viwili vya kifo vya nambari
mbili tofauti za usajili, ambavyo alinuia kutumia kudai fidia zingine.
Wapelelezi
walisema visa hivyo vinazidi kuongezeka huku walaghai wengi
wakishirikiana na maafisa wa bima kutayarisha malipo ya fidia bandia,
kutokana na mamilioni ya pesa zinazowekezwa katika sekta hiyo ya bima.
Kesi
zingine 10 zinazohusu wanandoa, zimeripotiwa na kuibua wasiwasi katika
kampuni za bima ambazo sasa zimeamua kuchunguza kiini hasa cha wateja
wanaowachukulia jamaa zao bima hususan 'za bei ghali’.
No comments:
Post a Comment