Usisahau Ubaharia Kisa Unahodha
HAYA tena Anti Naa mwenye maneno ya shombo nimekuja tena, sina tofauti na mnazi unaojiotea ufukweni ambao wakati wote upo tayari juujuu kuchungulia wale wanaovaa vinguo vifupi kudumbukia kwenye maji, hilo nalo neno!
Sina haja ya kukupa salamu maana mwenzio limenifika hapa! Nikisema hapa hata we unajua yaani shingoni kama siyo kwenye koromeo kabisa! Hakuna vitu vinavyokera kama kuwaiga wenzetu ati! Jitu zima linaingia hadi kazini ukiliangalia limevaa nguo safi mchunguze basi humo ndani alichovaa loo!
Chuki chukia, vimba uvimbiwe wala miye hunitishi, hunibabaishi ndiyo kwanza nasonga! Anti Naa chuma cha reli ukigusa lazima ugongwe, upo? Haya niambie mwanakwetu kutwa kuvaa boksa za kiume na wewe mwanaume kuvaa nguo za kike, inahu? Unasahau ubaharia kisa umepewa unahodha, unaona nguo za kiume zina dili unasahau na kuziacha zako!
Naongea na wewe mwanamke mwenzangu usiye na haya! Eti ooh napenda
kuvaa za kiume zinanipa uhuru! Unajua uhuru wewe? Ndiyo ulivyofundwa
uvae nguo za ndani za mumeo na mumeo avae za kwako? Si naongea na wewe
unayenitumbulia macho kama gari linaloshuka kwenye mteremko wa tope bila
breki! Haya tuseme umevaa hiyo nguo ya mkeo na kwenda nayo huko kwa
wanaume wenzako, bahati mbaya ukainama wenzako wakakuona utasema
umerogwa?
Wenzako waliozitengeneza walikuwa na akili zao ndiyo maana
zikaandikwa hii ya kiume na hii ni ya kike, hapa paja dogo hapa kubwa,
hapa mbele nakshinakshi hapa kamba tena kama kipofu wewe ukawekewa na
marinda kabisa kutofautisha! Sa dume zima umejipamba nje suti ndani
umevaa bikini, heee heee heeiya! Acha nicheke kwa hasira Anti Naa miye
maana nikinuna siku haziendi mwenzangu!
Nikugeukie na wewe mwanamke mwenzangu, mwanamke uliyefundwa ukapitia
ngazi zote tena wanakuita konkodi, ukachujwa ukachujika kweli wa kuvaa
nguo za ndani za kiume na kujisifu mtaani? Hata kama umeshauriwa
maana hushindwi kujitetea ‘ohh mimi mume wangu anapenda nivae’ hee huyo
mumeo kashushwa toka mbinguni! Mwanaume wa timilifu hawezi kupendezwa na
hiyo tabia, upo somo?
Shoga badilika mwenzangu, tena badilika na ufundike kweli! Nasema na
wewe kwa uso mpana wala sijitii ubaya! Mwana-mke uliyeka-milika huwezi
kujisifu kuvaa nguo za kiume tena ume-starehe kama upo peponi, koma tena
ukomae! Ngoja nikuulize kitu, hivi ukivaa hizo nguo unatembeaje huko
mtaani, haya ukienda maliwatoni kule ambapo mnakutana wengi kwenye
misiba na sherehe unavuaje maana jibu limenipitia kushoto mwenzenu!
Ushauri wangu wa bure ni kama maji usipokunywa basi nawa au uoge
kabisa! Mwanamke jitambue, usafi siyo kupendeza tu na kuoga mwenzangu,
usafi ni pamoja na nguo za ndani. Wanaume waachie zao na wao wajitambue
sasa! Kwa leo niishie hapa tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine
nzuri.
No comments:
Post a Comment