RAIS MAGUFULI AWATULIZA MACHINGA MWANZA
RAIS John Magufuli ametua jijini Mwanza
jana na kufunika kwa mapokezi makubwa huku akisema kwamba kamwe
hatakubali kuwaona wafanyabiashara wadogo nchini maarufu kama wamachinga
wakisumbuliwa na kushindwa kufanya biashara.
Aidha, amesema atahakikisha kuwa dhuluma
zilikuwa zinafanywa kwa wananchi wanyonge haziwezi kupata nafasi kwenye
serikali yake. Rais Magufuli aliyasema hayo muda mfupi wakati
alipowahutubia mamia ya wakazi wa Mwanza waliojitokeza kwa wingi
katikati ya Jiji la Mwanza kumlaki baada ya kuwasili jijini hapa kwa
ziara ya kikazi ya siku mbili.
Kabla ya kutoa hotuba yake katikati ya
Jiji la Mwanza akielekea Ikulu Ndogo ya Mwanza, Rais aliwapungia mkono
na kuwashukuru wakazi hao kwa mapokezi makubwa waliyoyaonesha kwake.
Alisema ndani ya uongozi wake
atahakikisha wananchi wa kati, wa juu na wanyonge wananufaika na
rasilimali za nchi, huku akiwataka Watanzania waendelee kuwa wamoja.
“Narudia hakuna machinga atakayesumbuliwa katika nchi hii, na ndio
kupitia Bunge tayari imetungwa sheria itakayowawezesha wamachinga
kupatiwa vitambulisho,” alifafanua na kuwataka Watanzania popote walipo
nchini waendelee kushikamana kwa kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la
kujiletea maendeleo na maisha bora.
Rais aliwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa
Mwanza saa 10.21 jioni na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John
Mongella, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenje, Katibu Mkuu wa
wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo, viongozi wa madhehebu ya dini na
mamia ya wananchi wa Jiji la Mwanza waliojipanga barabarani kutoka
uwanja huo hadi Ikulu wakimpungia mikono na vigelele vya furaha, huku
baadhi yao wakisikika kumtakia afya na maisha marefu.
Leo Rais anaendelea na ziara yake ya
kikazi wilayani Sengerema ambako atazindua rasmi mradi mkubwa wa maji wa
Nyamazugo uliojengwa kwa gharama ya Sh bilioni 20 ambao unatarajia
kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi 138,000 na kuwaondolea
tatizo la maji la muda mrefu.
IMEANDIKWA NA MAULID, MWANZA
No comments:
Post a Comment