Polisi wateketeza Wauaji wengine Kibiti
Jeshi la Polisi nchini limewaua watu wawili wanaodaiwa kufanya mauaji katika Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji, mkoani Pwani.
Akielezea tukio hilo leo (Alhamisi Julai 6) , Mkuu wa Operesheni
Maalumu za Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Liberatus
Sabas amesema tukio hilo lilitokea jana saa nne usiku katika msitu wa
Ngomboroni Kata ya Ikwiriri, Wilaya ya Ikwiriri.
Wahalifu hao waliuawa na askari wa operesheni maalumu wakiwa katika
doria za ufuatiliaji wahalifu sugu wanaojihusisha na mauaji
yanayoendelea katika kanda hiyo ya kipolisi.
Alisema askari wakiwa na mtuhumiwa mmoja muhimu anayeshiriki katika
mauaji hayo ambaye alikamatwa, alikubali kwenda kuwaonyesha polisi
mahali ambapo ni maficho ya wenzake.
“Baada ya kufika eneo la msitu wa Ngomboroni kikundi cha watu
wanaokadiriwa kufikia watano walikurupuka kutoka kwenye kichaka na
kuanza kukimbia ndipo polisi kwa tahadhari kubwa walianzisha
mashambulizi na kufanikiwa kumjeruhi mhalifu mmoja kwa risasi, katika
mashambulizi hayo mtuhumiwa aliyekuwa mkononi mwa polisi naye
alijaribu kutoroka na hivyo kupelekea kumjeruhi kwa risasi hivyo idadi
yao kufikia wawili,” amesema.
Ameongeza; “majeruhi hao wawili walifariki dunia njiani wakati
wakipelekwa hospitali kwa matibabu kutokana na kuvuja damu nyingi
iliyosababishwa na majeraha ya risasi waliyoyapata. Miili ya marehemu
imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili.”
Kamishna Sabas amesema katika tukio hilo wamefanikiwa kupokonya silaha
mbili aina ya SMG na Shotgun moja pamoja na risasi tisa.
Kamishina Sabas amewataka wananchi kutoa taarifa zitakazowezesha
kupatikana kwa wahalifu wengine waliosalia na kwamba zawadi nono bado
ipo pale pale na itatolewa kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa sahihi
kuhusiana na wahalifu wanaojihusisha na mauaji katika kanda maalumu ya
Rufiji.
No comments:
Post a Comment