Trending News>>

NALIAMSHA DUDEEE… KAZA CHAGA MAMA!

NILIKUWA kijiweni katika mishemishe zangu za kusaka ‘mpunga’ nilipopigiwa simu na dada anayekimbiza mtima wangu siku zote.
“Hallow baby,” nikaitika.
“Uko wapi honnie?” aliuliza kisha akaendelea kuzungumza, “nipo nyumbani kwako, nina masaa mawili ya kukusubiri.”
Mwili ulisisimka, nikajibu kwa pupa, “Sikia, dude langu limeshaamka, chukua funguo kwa Mama Ndambi hapo mlango wa pili, ingia ndani, kaza chaga kabisa nafika sasa hivi.”
“Sawa, ila ukichelewa nitaondoka, sikai sana,” alijibu, akakata simu.
Kwa wakati huo nilikuwa Bagamoyo. Nyumbani kwangu alikokuwa mrembo yule ni Mbagala. Niliwaza njia itakayonifikisha kwa haraka, nilisahau kazi iiyonipeleka Pwani, kweli aliumbwa Adamu, alipokuja Hawa akaharibu kila kitu. Wanawake wanasumbua ndugu yangu.
Nilitamani kukodi ndege binafsi ili niwahi kufika, lakini kwa hali yangu ya kiuchumi, sikuwa na jeuri hiyo. Mimi ni fukara mtiifu, fedha ilinipiga chenga, nikaenda kwa waganga kusafisha nyota, waganga wakashindwa, wakanyoosha mikono hoi taabani. Nyota chafu!
Nilipata wazo la kupanda gari, hata hivyo, suala la foleni lilinikatisha tamaa. Akili ikazama katika dimbwi la mawazo, nikaibuka na ‘new idea’, nitafute pikipiki. Haraka, nikamfuata Mudi rafiki yangu dereva bodaboda ambaye hakuwa mbali na mahali nilipokuwa.
“Mudi niazime pikipiki yako kuna mahali nawahi,” niliomba.
“Unajua kuendesha pikipiki wewe?” alihoji.
“Nifundishe, hata wewe walikufundisha asubuhi, mchana ukabeba abiria, pikipiki ‘simpo’ bwana!”
Mudi aliniamini sana, akanipa maelekezo, “Unaiona hii… inaitwa ‘krach’, hii ‘breki’, huu moto unaongeza ‘spidi’, hapa kuna gia…”
Alinielekeza nikamwelewa. Akanipa chombo, niwahi katika jambo langu!
Sasa nilikuwa barabarani nikiendesha pikipiki. Walioniona walishika mikono kichwani kwa kasi niliyokuwa nayo. Kila nilipopita niliacha mishangao, ngurumo na vumbi!
Wakati nikiwa ‘spid 120’ katika pikipiki ile ya kuazima, mbele nikaliona lori la mizigo, nika-’ovateki’, nikakutana na kona, nikafanikiwa kukunja, barabara ikanyooka, nikaongeza kasi maradufu.
Ghafla mbele yangu niliona kundi la wanyama wakivuka barabara, nikataka kusimama, lakini sikukumbuka breki ilikuwa upande gani, hata kama ningekumbuka, nilikwishachelewa. GIZA!
Nilipata fahamu siku mbili baada ya tukio… nilikuwa katika hospitali nisiyoikumbuka jina nikiponywa majeraha ya kujitakia.

Naliamsha dudeee… kaza chaga mama!

No comments:

Powered by Blogger.