Mbowe amjibu Polepole kuhusu kigogo wa Chadema anayetarajiwa kuhamia CCM
Mwenyekiti
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amejibu
kauli iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey
Polepole aliyesema kuna mtu mzito wa Chadema atakayehamia chama tawala
hivi karibuni.
Mbowe
amesema kuwa Chadema haiwezi kutetereka kwa kuondoka kiongozi yeyote
kwani imejengwa katika misingi imara kama taasisi isiyotegemea mtu.
“Kwanza
kabisa sitaki kuzungumzia propaganda za Polepole ambaye najua
anajifunza siasa. Wapo wazito zaidi waliohama au kufukuzwa. Lakini
niseme tu chama hiki kina misingi yake, mtu awe mdogo au mkubwa ni
tafsiri tu, ingawa wapo wenye mchango mkubwa,” Mbowe anakaririwa na
Mtanzania.
“Mtu
yoyote anaweza kuondoka lakini Chadema kama taasisi itabaki imara. Mimi
kama Mwenyekiti ninajua tumejenga taasisi imara ambayo haiwezi
kutetereka kwa wanachama au kiongozi wa ngazi yeyote kuondoka,”
aliongeza.
Kauli
hiyo ya Mbowe imekuja wakati ambapo kumekuwa na matukio ya madiwani wa
Chadema kuhamia CCM katika mikoa ambayo inasadikika kuwa ni ngome ya
chama hicho kikuu cha upinzani kama Arusha na Kilimanjaro.
Mwenyekiti
huyo wa Chadema ambaye pia ni Mbunge wa Hai amesema kuwa walifahamu
hatua za madiwani hao zaidi ya 10 kufanya kile alichokiita usaliti hata
kabla hawajatangaza kuhama.
No comments:
Post a Comment