MAJALIWA: HAKUNA KIJIJI TANZANIA KITAKACHOACHWA BILA YA UMEME
MAJALIWA: HAKUNA KIJIJI TANZANIA KITAKACHOACHWA BILA YA UMEME
*Asema vilivyo mbali na gridi kufungwa sola
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema hakuna kijiji nchini kitakachoachwa bila ya kuunganishiwa umeme
katika awamu ya tatu ya Mradi wa Nishati Vijijini (REA).
Amesema Serikali imetenga
shilingi trilioni moja kwa ajili ya kusambaza umeme katika vijiji 8,000
ambavyo bado havijaunganishiwa nishati hiyo.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo
jana jioni (Jumanne, Julai 11, 2017) alipozungumza kwa nyakati tofauti
na wananchi wa wilaya ya Ruangwa.
Waziri Mkuu ambaye ameambatana na
mkewe Mama Mary Majaliwa aliyasema hayo katika mikutano aliyoifanya
kwenye vijiji vya Chiapi, Nandanga, Mbecha na Luchelegwa, ikiwa ni siku
ya pili ya ziara yake ya kikazi ya siku nne Mkoani Lindi.
“Rais wetu Dkt. John Magufuli
anajali sana wananchi wake, hivyo ametenga fedha nyingi
zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote vikiwemo na wilaya
ya Ruangwa. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu.”
Pia Waziri Mkuu amesema
mwananchi hawatowajibika tena katika kulipia nguzo wala fomu za maombi
ya kuunganishiwa umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zimeshabebwa na
Serikali.
Waziri Mkuu aliongeza kwamba
lengo la Serikali ni kufikisha umeme kwenye vijiji vyote Tanzania na
kwa vile ambavyo viko kwenye maeneo yaliyo mbali na gridi vitafungiwa
sola, jambo ambalo litafungua fursa za ajira na kukuza uchumi.
Waziri Mkuu alisema huduma hiyo
ni muhimu kwani mbali ya kutumiwa majumbani lakini pia kwa kusogezwa
karibu na maeneo ya pembezoni itawezesha zahanati,shule ,viwanda na
vituo vya afya kuwa na umeme.
Kwa upande wake Meneja wa Tanesco
Mkoa wa Lindi Mhandisi, Johnson Mwigune alimuhakikishia Waziri Mkuu
kwamba hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu mkandarasi aliyepangiwa
katika vijiji hivyo atakuwa tayari ameanza kazi ya kusambaza umeme
No comments:
Post a Comment