KIJANA AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KULAWITI WANAFUNZI WA SHULE YA MSINGI
HALID Mohamed (28) amefikishwa Mahakama
ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Igunga kwa tuhuma ya kulawiti wanafunzi
wawili wa shule ya msingi Chipukizi wilayani Igunga mkoani Tabora.
Mwendesha Mashitaka wa Polisi Wilaya ya
Igunga, Elimajid Kweyamba aliiambia mahakama mbele ya hakimu wa mahakama
hiyo, Ajali Milanzi kuwa shitaka la kwanza linalomkabili mshitakiwa
huyo lilitokea kati ya Februari 1 mpaka 14 mwaka huu.
Alisema katika Mtaa wa Uarabuni mjini
Igunga mshitakiwa alimlawiti mwanafunzi mwenye miaka 9 wa kiume
anayesoma darasa la pili shule ya msingi Chipukizi na kumsababishia
maumivu makali sehemu zake za siri.
Aliongeza kwamba shitaka la pili
lilitendeka kati ya Februari 1 hadi 14 vilevile katika mtaa huohuo
ambapo mshitakiwa alimlawiti mwanafunzi wa miaka 7 wa kiume anayesoma
darasa la pili katika shule hiyo hiyo ya Chipukizi.
Alisema mshitakiwa alitenda makosa hayo
mawili kinyume na kifungu 154 kidogo cha kwanza (a) (2) kanuni ya adhabu
sura ya 16 mapitio ya 2002 inayozuia kutenda makosa kama hayo.
Baada ya kusomewa makosa hayo mawili
mshitakiwa alikana kutenda makosa hayo yote mawili ambapo yuko nje kwa
dhamana ya Sh milioni 4 kwa makosa yote mawili na kesi hiyo imeahirishwa
hadi Julai 17 mwaka huu wakati kesi itakapoanza kusikilizwa
IMEANDIKWA NA LUCAS RAPHAEL,- HABARILEO -IGUNGA
No comments:
Post a Comment