JIFUNZE KUONA CHANGAMOTO KWA JICHO LA FURSA.
Siku moja ikiwa ni miaka mingi ya nyuma iliyopita, palitokea ndugu
wawili waliokuwa marafiki waliopata nafasi ya kutembelea nchini India
kwa kufanya utalii nchini humo. Walipokuwa wakitembea katika mitaa
mbalimbali ya mji wa Bombay walishangaa sana kuona maelfu ya watu
waliokuwa masikini wamezagaa na kukaa kila kona ya njia za mitaa ya mji
huo. Baadhi ya watu walionekana wamekaa chini ya madaraja na mabakuli ya
kuombea msaada, na wengi wao zaidi wakizunguka katika mitaa hiyo huku
wakionekana ni watu wasiojiweza kabisa (masikini sana) tena wakiwa
pekupeku pasipo kuvaa viatu.
Mmoja wa wale marafiki wawili waliokuwa wakitembea pamoja akamwambia
mwenzake, “angalia hao watu. Wanatia huzuni sana?” Wanatembea bila
viatu. Na tena ni watu wengi (maelfu ya watu). Hii inatia huruma sana.
Na pia ni aibu kubwa kwa taifa kama letu tulikotoka ambako kuna kila
aina ya viatu vingi vya kuweza kuwasaidia hawa watu tunaowaona huku
wakitembea pasipo viatu. Sitasahau jambo hili nililoliona kwa macho
yangu kwani linatia huruma. Akamalizia kwa kusema, “nitakaporudi
nyumbani (nchini mwake) nitamsimulia mke wangu kuhusu kisa hiki
nilichokiona.” Ndugu huyu aliendelea kuongea mambo mengi kuhusu namna
alivyoona masikini wanavyotembea pekupeku pasipo viatu miguuni mwao.
Kwa muda huo yule rafiki yake alikuwa ameamua kuchukua kipande cha
karatasi na akaweza kuandika mambo baadhi aliyokuwa ameyaona katika mji
ule. Baada ya hapo alivyorudi nchini mwake Marekani moja kwa moja
alianza kufatilia kwa karibu mkakati ule aliouandika na namna gani
atakavyoweza kusafirisha viatu kutoka nchini mwake kupeleka nchini
India, na namna gani ya kuweza kutengeneza kiwanda na kuzalisha viatu
moja kwa moja akiwa huko huko nchini India.
“Ukiona Mungu ameruhusu uone tatizo
lililoko kwenye mazingira yaliyokuzunguka ujue ameona unao uwezo mkubwa
ndani yako aliouweka wa kuitua changamoto hiyo.” -EZEKIEL MANYAMA
Hebu tazama tofauti ya watu hawa wawili, wa kwanza anawaza na kusema,
“angalia watu hawa wanavyotembea peku peku pasipo kuvaa viatu na kisha
kuwaonea huruma tu,” Huyu wa pili yeye aliamua kusema, “nikitazama hawa
watu miguuni ni wazi kabisa wanahitaji viatu.” Hii ni wazi wote wawili
walikuwa na macho ya kuona changamoto na tatizo lile lakini ni wazi pia
kila mmoja aliona na kuchukulia changamoto Ile kwa namna ya tofauti.
Mmoja aliona ni tatizo kama tatizo na kuishia kuwaonea huruma watu wale,
mwingine aliona changamoto kama FURSA ya kutatua ili kuwasaidia watu
wale wa mji wa Bombay na zaidi sana kwa kupitia changamoto ile, yeye
aweze kufanikisha maono ya kile alichokuwa anakiona ndani yake.
Leo hii ndugu huyu ameweza kufungua biashara kubwa na kuwa na kampuni
mojawapo kubwa inayohusika na uzalishaji wa viatu nchini Marekani.
Mmoja aliona miguu isiyo na viatu na kubaki kuongea pasipo kuchukua
hatua yoyote kivitendo. Na mwingine aliona fursa ya kibiashara kupitia
miguu isiyokuwa na viatu. Hii ni wazi kabisa tukisema, Maisha ni vile
unavyowaza na kuona ndani yako na hapo ndivyo utakavyofanikiwa. Ni wazi
ukiwa mwenye Maono makubwa ndani yako ukaunganisha na Imani ndogo
uliyonayo, utaona kila changamoto unayokutana nayo kama fursa ya kipekee
ya kukusaidia kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine na si kikwazo cha
kukukwamisha mahali ulipo.
Ili ufanikiwe kwenye maisha yako unahitaji kuona changamoto
unazokutana nazo kila mara kama fursa iliyoficha utajiri mwingi ndani
yake na si kuishia kuongelea na kuikimbia changamoto yenyewe. Ukiona
Mungu ameruhusu uone tatizo lililoko kwenye mazingira yaliyokuzunguka
ujue ameona unao uwezo mkubwa ndani yako aliouweka wa kuitua changamoto
hiyo. Ile kuishi duniani tu, unapaswa kutambua bado Mungu anataka
ujifunze kuona changamoto kama fursa unazotakiwa kuzitatua. Moja ya
sababu iliyotuleta duniani kuishi, ni kutatua changamoto ili kuleta
majibu kwa watu na dunia tunayokaa. Amini unauwezo mkubwa wa kufanya
makubwa kuzidi yale yaliyokwisha kufanyika hapo nyuma.
1 comment:
Waw its a good news
Post a Comment